Kimataifa

Jude Bellingham Kumshawishi Trent Kuhamia Real Madrid

Jude Bellingham Kumshawishi Trent Kuhamia Real Madrid

Habari kuhusu uhamisho wa beki wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold, kwenda Real Madrid katika dirisha la usajili wa majira ya kiangazi zimepamba moto zaidi. Hii inakuja baada ya kuonekana akiwa na staa wa mabingwa hao wa Hispania, Jude Bellingham, kwa mara nyingine jijini Los Angeles, Marekani wiki hii.

Alexander-Arnold, ambaye kwa sasa ni nahodha msaidizi wa Liverpool, amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake na klabu hiyo. Ingawa kuna mazungumzo yanayoendelea kati yake na mabosi wa Liverpool, bado hawajafikia muafaka.

Katika hali hii ya sintofahamu, taarifa zimeibuka kwamba Real Madrid inamuwania beki huyo na inamtumia Bellingham kama sehemu ya ushawishi. Hii ni kwa sababu Bellingham ni rafiki yake wa karibu na wote wanaichezea timu ya taifa ya England.

Wakiwa mapumzikoni Marekani, Alexander-Arnold na Bellingham wameonekana pamoja mara kadhaa. Mapumziko haya yalitokana na ruhusa waliyopewa kutokana na kuichezea England katika michuano ya kimataifa. Urafiki wao, ulioanza walipokutana kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa, unaweza kuwa sababu muhimu kwa Trent kukubali kujiunga na Real Madrid.

Real Madrid inaamini kwamba urafiki wa muda mrefu kati ya Bellingham na Alexander-Arnold unaweza kushawishi beki huyo kukubali ofa yao ya kujiunga na timu hiyo katika dirisha hili la usajili. Hata hivyo, kama mpango huo hautafanikiwa sasa, mabosi wa Real Madrid wamepanga kusubiri hadi mwisho wa msimu ujao ili kumsajili bure, kama walivyofanya na Kylian Mbappe aliyejiunga nao baada ya mkataba wake na PSG kumalizika.

Liverpool, kwa upande wake, inapambana kumshawishi Trent asaini mkataba mpya. Lakini kama akikataa, kuna uwezekano mkubwa kwamba klabu hiyo inaweza kumuuza ili asije kuondoka bure au kwa bei ndogo katika dirisha la usajili la majira ya baridi mwakani.

Leave a Comment