Kimataifa

Nabi Moto Chini Kaizer, Yanga Yatoa Kichapo Cha Magoli 4-0

Nabi Moto Chini Kaizer, Yanga Yatoa Kichapo Cha Magoli 4-0

Mashabiki wa Kaizer Chiefs nchini Afrika Kusini wameanza kumkataa kocha wao mpya, Nasraddine Nabi, baada ya timu hiyo kupokea kipigo kizito cha 4-0 kutoka kwa Yanga. Mechi hiyo iliyochezwa hivi karibuni ilishuhudia Yanga ikishinda kupitia mabao ya Prince Dube, Aziz Ki (mabao mawili), na Clement Walid Mzize.

Junior Kanye, mchezaji wa zamani wa Kaizer Chiefs na mchambuzi wa soka, ametoa maoni yake akisema mashabiki wa Kaizer Chiefs wanahitaji kuelewa hali halisi ya soka. Alieleza kuwa Yanga ni moja ya timu bora zaidi barani Afrika kwa sasa na kwamba Kaizer Chiefs bado inajijenga.

“Mashabiki wa Kaizer Chiefs wanapaswa kuelewa kuwa Young Africans ni timu bora Afrika kwa sasa. Kaizer Chiefs bado inajitafuta,” alisema Junior Kanye. Aliendelea kusema kuwa alitarajia matokeo hayo tangu mwanzo wa mashindano ya Toyota Cup, akiongeza kuwa Yanga ina wachezaji wenye nguvu kiakili na uzoefu wa kucheza katika mashindano makubwa kama CAF.

Junior Kanye aliendelea kusema, “Yanga wameweza kuifunga Simba (5-1), timu iliyo kwenye kumi bora ya CAF. Hivyo, si ajabu kwa Kaizer Chiefs kufungwa 4-0. Yanga ni mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo mashabiki wanapaswa kupunguza matarajio yao.”

Alisisitiza kuwa mashabiki wa Kaizer Chiefs wanapaswa kuelewa kuwa mafanikio yanahitaji muda. “Nabi na benchi lake la ufundi wanahitaji zaidi ya misimu miwili kuitengeneza Kaizer Chiefs kuwa timu bora,” alihitimisha Junior Kanye.

Leave a Comment