Kimataifa

Willy Onana Afunga Mlango wa Qatar, Akimbilia Libya

Onana Afunga Mlango wa Qatar, Akimbilia Libya

Willy Essomba Onana, aliyekuwa mshambuliaji wa Simba kutoka Cameroon, anakaribia kukamilisha mkataba wake na klabu ya Al Ahli Benghazi ya Libya baada ya mpango wake wa kujiunga na Muaither ya Qatar kufeli.

Onana, ambaye alifunga mabao manne msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, alikuwa na matarajio ya kuhamia Muaither inayoshiriki Ligi ya Qatar (Qatar Stars League). Hata hivyo, mkataba huo umekwama na sasa atajiunga na Al Ahli Benghazi.

Mshambuliaji huyu alifanya maandalizi ya msimu mpya (‘Pre Season’) na Simba jijini Ismailia, Misri, kabla ya kutolewa dakika za mwisho ili kumpisha kipa Moussa Camara kutoka AC Horoya. Camara aliletwa kuchukua nafasi ya Ayoub Lakred, ambaye aliumia akiwa na timu wakati wa maandalizi ya msimu mpya.

Kipa Ayoub aliletwa kwa ajili ya kuongeza nguvu katika eneo la kipa, baada ya viongozi wa Simba kuonyesha kutokuwa na imani na makipa wengine wa ndani, Hussein Abel na Ally Salim, ambao walishindwa kutoa ushindani wa kweli.

Onana, alijiunga na Simba Julai 5, mwaka jana akitokea Rayon Sports ya Rwanda, ambapo alikua mfungaji bora kwa kufunga mabao 16 na kuasisti mengine matano. Hata hivyo, licha ya kuwa mchezaji bora wa msimu katika Ligi Kuu ya Rwanda (MVP), hakufanikiwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa na aliondolewa kwenye kikosi cha Simba kwa sababu ya kigezo cha wachezaji 12 wa kigeni.

Kama ilivyokuwa, Onana anaondoka Simba baada ya msimu wa kihistoria, akiondoka kwa matumaini ya mafanikio mapya nchini Libya.

Leave a Comment