Simba SC

Simba Day 2024: Wazee Simba Wafunguka na Kutoa Pongezi kwa Uongozi

Simba Day 2024 Wazee Simba Wafunguka na Kutoa Pongezi kwa Uongozi

Simba Day 2024: Sherehe za Simba Day Zawaleta Pamoja Wapenzi na Wazee wa Simba

Simba Day inayofanyika kesho itakuwa ya 16 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009 chini ya uongozi wa Hassan Dalali ‘Field Marshal’ na Mwina Kaduguda.

Katika msimu mpya wa Simba Day yenye kauli mbiu ya “Ubaya Ubwela,” Mwanaspoti imefanya mahojiano na wazee na viongozi wa zamani wa klabu hiyo, akiwemo Dalali, ambao wamepongeza uongozi wa sasa kwa kusimamia tamasha hilo na kuona likizaa matunda makubwa.

Muasisi Dalali anasema anajisikia faraja kuona tamasha hilo linafanyika kila mwaka ambapo linawaleta wana Simba pamoja ili kurudisha shukrani kwa jamii na kutambulisha wachezaji wa msimu mpya.

“Kwa asilimia kubwa malengo ya tamasha hilo yanafanyika, ingawa ninachotamani kuona ni kumalizika kwa uwanja wa Bunju na mechi kuchezwa pale, hilo ndilo ninalotamani kulishuhudia nikiwa hai.”

“Ninachotarajia kwenye tamasha hilo ni kufurahia kuona Wanasimba tunakusanyika kwa pamoja na kuwatakia kila lakheri wachezaji wetu, kupigania ubingwa wa msimu ujao.”

Dalali anasema kupitia tamasha hilo, wachezaji wapya wa Simba watatambua majukumu makubwa yaliopo mbele yao kutokana na umati wa watu utakaofurika uwanjani.

“Wapenzi wa Simba kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na nje watawapa taswira wachezaji ama kuwaachia deni la kuhakikisha msimu ujao wanachukua ubingwa, kutokana na ukarimu ambao wataonyeshwa Simba Day,” anasema.

Kuhusiana na mechi ambayo Simba inatarajia kucheza dhidi ya APR ya Rwanda, Dalali anatarajia kuona vipaji vikubwa kutoka kwa wachezaji wapya na waliopo, kwani anaamini viongozi wamefanya kazi nzuri ya usajili.

“Simba imebadilisha kwa kiasi kikubwa kikosi chake, na nilichopenda ni kuwasajili vijana ambao wana hamu ya mafanikio. Hivyo naamini msimu unaokuja utakuwa wa kicheko kwetu,” anasema.

Abdallah Kibadeni, mchezaji na kocha wa zamani wa timu hiyo, anasema anatamani katika tamasha hilo wazee waliotumia muda mwingi kuitumikia klabu watambuliwe.

“Kuna wazee wengi ambao waliitumikia Simba kwa nyanja mbalimbali. Hao watambuliwe katika tamasha hilo. Wapo wengi kama Dalali, Kaduguda, nipo mimi na wengine wengi, ili kuonyesha vizazi vijavyo kwamba wanahitaji kuwa wazalendo kwa klabu yao,” anasema.

Ally Pazi Samatta, mchezaji wa zamani wa Simba, anasema anatarajia kuona mambo mengi mazuri katika tamasha hilo na anashauri uongozi ufanye kitu kwa ajili ya Dalali.

“Dalali na Kaduguda ndio waanzilishi wa tamasha hilo, linalowapa raha mashabiki wa Simba. Kama haitoshi, Yanga imeiga kutoka Simba nayo inafanya vizuri. Hilo litoshe kwa viongozi wa Simba kuwaza kufanya kitu kwa watu hao, ikiwezekana serikali iwaone maana wameleta furaha kwa Watanzania,” anasema.

Leave a Comment