Simba SC

Kocha Fadlu Abaini Changamoto za Simba

Kocha Fadlu Abaini Changamoto za Simba

Baada ya kuongoza Simba kupata ushindi wa pili mfululizo katika mechi za kirafiki, Kocha Mkuu Fadlu Davids ameeleza furaha yake kuhusu jitihada za wachezaji na uwezo wao wa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga. Hata hivyo, ameainisha kuwa bado kuna changamoto kubwa ambayo anahitaji kushughulikia kabla ya msimu mpya kuanza.

Katika mchezo uliochezwa hivi karibuni, Simba ilishinda 2-1 dhidi ya Telecom Egypt FC, ikiendeleza mfululizo wa ushindi baada ya kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya El-Qanah. Kocha Fadlu alisisitiza kuwa kama mastraika wake wangeonyesha umakini zaidi, Simba ingeshinda kwa mabao 7-1.

Fadlu alieleza kwamba wachezaji walicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi, lakini mastraika walishindwa kufunga mabao ya wazi, jambo ambalo alidai anahitaji kulifanyia kazi kabla ya michuano ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika kuanza.

“Tulikuwa na nafasi nyingi za kufunga mabao sita hadi saba, lakini hatukufanikiwa kuzitumia vizuri, huku wapinzani wetu walipata nafasi moja tu na kufunga. Kinachotakiwa ni wachezaji kukimbia kwa wakati na kumalizia nafasi za kufunga kwa usahihi,” alisema Fadlu, ambaye ni kocha kutoka Afrika Kusini na alihamia Simba kutoka Wydad Casablanca ya Morocco.

Kocha huyo aliongeza kuwa timu imeimarika na wachezaji wanaonyesha ushindani mzuri kwa nafasi kwenye kikosi cha kwanza. “Nafurahia namna wachezaji wanavyofanya kazi na kuonyesha uwezo wao. Michezo miwili ya kirafiki iliyoonyesha mambo mengi mazuri na kutufanya kuwa na matumaini ya kufikia malengo yetu,” alisema.

Fadlu pia alizungumzia mchezo wa kirafiki ujao katika Simba Day na kusema, “Michezo hii ya kirafiki ni muhimu sana, kuna mambo tumeandaa kwenye kambi yetu ambayo mashabiki watayaona.”

Kocha huyo aliongeza kuwa kikosi kitarejea nchini kesho jioni kwa ajili ya maandalizi ya tamasha la Simba Day. “Tunaendelea na maandalizi yetu ya mwishoni mwa ‘pre season’. Tutaanza kurejea Jumanne jioni baada ya mazoezi mengi kwenye ufundi, mbinu, kasi na utimamu wa mwili,” alisema.

Katika mchezo wa hivi karibuni, Simba ilianza kwa kushindwa, lakini ilirejea kwa nguvu kipindi cha pili na kufunga mabao mawili kupitia Mashaka Valentino, aliyesajiliwa msimu huu kutoka Geita Gold, na Ladack Chasambi. Valentino alisema kwamba maelekezo ya kocha yaliwezesha kufunga bao la kusawazisha.

“Mchezo ulikuwa mgumu, lakini mwalimu aliniambia niwe katika eneo sahihi kwenye lango, na kwa kufanya hivyo nilifanikiwa kufunga,” alisema Valentino.

Chasambi, aliyefunga bao baada ya pasi nzuri kutoka kwa Kelvin Kijili, alieleza kuwa ilikuwa ni moja ya mabao bora aliyowahi kufunga.

Simba ilitarajiwa kucheza mechi yao ya mwisho jana usiku dhidi ya Al-Adalah FC katika Uwanja wa New Suez Canal, timu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Saudi Arabia.

Leave a Comment