Soka

Yusuf Kagoma: Ndoto za Udaktari Hadi Uchezaji Mpira

Yusuf Kagoma: Ndoto za Udaktari Hadi Uchezaji Mpira

Ndoto Za Yusuf Kagoma: Udaktari Hadi Kucheza Mpira

Yusuf Kagoma, anayependa jezi namba 21, ameeleza changamoto alizokutana nazo katika kufanya maamuzi ya kujiunga na Simba baada ya kuwa tayari amesaini mkataba wa awali na Yanga.

“Haikuwa rahisi kwani mambo yalikuwa mengi lakini ukweli nilikuwa naujua mimi mwenyewe. Yanga sikusaini kama watu walivyodhani, bali walileta ofa kama ilivyo Simba,” Kagoma anaeleza.

“Mara baada ya Simba kunitangaza kuwa mchezaji wao nilipumua kwa sababu nilikuwa nalisubiri hilo kwa hamu ili kuepukana na changamoto za simu nyingi na maoni mengi ya wadau,” Kagoma anasema.

Kagoma anasisitiza kuwa alisaini mkataba na Simba tu.

“Mimi nilifahamu ukweli wa mambo. Ni kweli nilikuwa na ofa kutoka Yanga ambao walikuwa wa kwanza kunifuata, lakini Simba walifanya haraka na kuweka ofa mezani, wakionyesha uhitaji wa dhati,” anaeleza kiungo huyo.

AUCHO, KAGOMA URAIA TU

Licha ya mastaa wengi wa kigeni kuja Tanzania na kutoa changamoto kwa mastaa wa nyumbani, Kagoma amesema hakuna tofauti kubwa ya ubora baina ya viungo wazawa na wageni.

“Tanzania imebarikiwa na vipaji vingi vya wachezaji, hasa nafasi ya kiungo. Ukifuatilia Ligi Kuu Bara unaweza kukubaliana nami kwani wachezaji wengi wanaofanya vizuri ni katika nafasi ya kiungo,” Kagoma anasema.

“Pamoja na timu kubwa kuwa na wachezaji wa kigeni kwenye nafasi hizo, bado wanawachanganya na wazawa ambao pia wameonyesha uwezo mkubwa na wa kuvutia, huku wakitajwa zaidi midomoni mwa watu,” anaongeza Kagoma.

Anasema utofauti upo kwa sababu binadamu wanatofautiana; mmoja anaweza kuwa na kitu cha kipekee na mwingine asiwe nacho, lakini kwa kiasi kikubwa wazawa wameamka na kuonyesha kuwa wanaweza.

DAKTARI HADI SOKA

Kagoma anafichua kuwa alikuwa na ndoto za kuwa daktari lakini hazikutimia kwa sababu ya soka.

“Ndoto yangu ilikuwa kuwa daktari. Nakumbuka tangu nikiwa shule, nikiulizwa unasoma ili uwe nani, jibu lilikuwa ni kuwa daktari ili niweze kuwatibu wagonjwa,” Kagoma anasema.

“Lakini soka lilichukua nafasi kubwa zaidi ya masomo. Pamoja na kufanikiwa kumaliza kidato cha nne, sikuweza kutimiza ndoto yangu ya udaktari na kujikuta nikiwekeza nguvu zaidi kwenye mpira ambao pia nilikuwa naupenda,” anamalizia kiungo huyo.

Leave a Comment