Yanga SC

Yanga Yapata Ushindi Mahakamani Dhidi ya Mzee Magoma

Yanga Yapata Ushindi Mahakamani Dhidi ya Mzee Magoma

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imetoa hukumu katika kesi iliyokuwa ikiikabili Klabu ya Yanga na Juma Ally Magoma pamoja na wenzake. Siku ya hukumu awali ilikuwa imepangwa kufanyika Jumatano, lakini iliahirishwa hadi leo baada ya wakili wa upande wa Mzee Magoma, Geofrey Mwaipopo, kushindwa kufika mahakamani.

Yanga yashinda kesi dhidi ya Mzee Magoma

Katika hukumu hiyo, Mzee Magoma na wenzake walipoteza kesi waliyoifungua wakipinga uhalali wa Baraza la Wadhamini la Yanga. Wakili wa Klabu ya Yanga, Simon Patrick, alifafanua kuwa mahakama imekubaliana na hoja tatu muhimu zilizowasilishwa na Yanga.

Kwanza, Mahakama ya Kisutu ilikubaliana na hoja kwamba haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, kwani kwa mujibu wa sheria, masuala ya uhalali wa Baraza la Wadhamini yanapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania. Hii ilipelekea kufutwa kwa hukumu ya awali.

Pili, mahakama ilipinga hoja kwamba Magoma hakuwa mwanachama halali wa Yanga wakati akifungua kesi hiyo. Mahakama ilisema suala hilo linahitaji ushahidi wa kutosha ili kuweza kusikilizwa.

Tatu, mahakama ilikubaliana kwamba Mama Fatuma Karume na Mzee Jabiri Katundu walinyimwa haki ya kusikilizwa. Watu waliowakilisha wawili hao mahakamani walikutwa hawakuwa na mamlaka kisheria, jambo lililopelekea kufutwa kwa hukumu hiyo.

Zaidi ya hayo, Wakili Simon alieleza kuwa mahakama pia iligundua kuwa maombi yaliyowasilishwa na upande wa Magoma yalifanywa kwa njia isiyo sahihi, kwa kutumia ‘petition’ badala ya ‘plaint’, na hivyo kupelekea kufutwa kwa kesi hiyo.

Kutokana na matumizi ya gharama kubwa na wanasheria wa Yanga katika kesi hii, Mahakama imeamua kuwa Mzee Magoma na wenzake wanatakiwa kulipa gharama za usumbufu ambazo zinaweza kufikia kati ya shilingi milioni 70 hadi 100.

Leave a Comment