Soka

Simba Wakubali Matokeo, Lakini Hawajakata Tamaa!

Simba Wakubali Matokeo, Lakini Hawajakata Tamaa!

Simba SC wapokea kichapo cha tatu mfululizo kutoka kwa Yanga, lakini wanapongezwa kwa kuonyesha kuwa wako tayari kwa mchakato wa muda mrefu kufikia ubora.

HAKIKA SIMBA WANAKUA… HONGERENI!

Simba imeonyesha maendeleo makubwa katika usajili wao wa msimu huu, na ishara zinaonyesha wako kwenye mwelekeo wa kufikia kiwango cha ubora ambacho Yanga wamekuwa nacho kwa takribani misimu mitatu sasa. Yanga wamejijengea umahiri wao, kiasi kwamba timu yoyote inayotaka kujitathmini kwa ubora ni lazima icheze dhidi yao kwanza.

Ubora wa Yanga umeonekana wazi hata katika michuano ya kimataifa, ambapo hawachezi kwa bahati, na hawajachoka kutafuta ushindi. Ni jambo la kupendeza kuona Simba wakikubali matokeo kwa mikono miwili, kwani huo ndio uanamichezo halisi! Kukubali kushindwa ni hatua ya kwanza muhimu kuelekea kuwa bora zaidi.

Haikuwahi kuwa rahisi kwa mashabiki wa Simba kujipongeza baada ya kufungwa na watani wao kwa mara ya tatu mfululizo. Lakini tafsiri ya hali hii ni kwamba sasa wameanza kuishi kwa uhalisia na kuamini katika mchakato wa muda mrefu badala ya njia za mkato. Simba sasa wanaamini wamepunguza pengo kati yao na Yanga, na matarajio yao ni kwamba muda si mrefu watafikia kiwango cha juu kama Yanga.

Swali muhimu ni je, Yanga watasalia katika ubora wao wa sasa, au wataweza kuongeza kiwango chao zaidi? Watu wengi wanajisahau kwamba Yanga nao bado wanaendelea kufanyia kazi ubora wao, hasa kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika. Hii ina maana kwamba kocha Gamondi Muguel na wachezaji wake wana kazi kubwa mbele yao kuhakikisha wanazidi kuwa bora zaidi.

Wapinzani wa Yanga wanahitaji kufanya kazi ya ziada ili kuweza kuwashinda, lakini hilo si jambo la haraka. Ni mchakato wa muda mrefu unaohitaji uvumilivu na bidii kubwa.

Ameandika David Kampista.

Leave a Comment