Simba SC

Simba SC yaandaa Maajabu kwenye Ngao ya Jamii

Simba SC yaandaa Maajabu kwenye Ngao ya Jamii

Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davies, amepanga sapraizi kubwa kwa mashabiki wakati wa mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga itakayofanyika Alhamisi, Agosti 8, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Baada ya kumaliza tamasha la Simba Day Jumamosi iliyopita, kocha Fadlu aliwapa mapumziko wachezaji wake huku akiwaagiza wachezaji kuangalia mechi ya Yanga dhidi ya Red Arrows iliyopigwa kwenye kilele cha Wiki ya Wananchi. Alisisitiza umuhimu wa kuifuatilia Yanga kwa makini kwani ndio mpinzani wao katika mchezo wa Ngao ya Jamii.

Wachezaji wa Simba walifuata maelekezo hayo, wakitazama mechi kwa makundi mbalimbali; baadhi walikuwa hotelini Dar es Salaam na wengine majumbani. Mmoja wa wachezaji alisema, “Tuliambiwa kuangalia mechi, wapo waliokuwa hotelini kwa pamoja lakini wengine tulikuwa majumbani.”

Kocha Fadlu na benchi lake walitazama mechi hiyo kwa undani zaidi, wakichambua mbinu za Yanga. Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally, alisema wameridhishwa na kikosi kipya cha Simba na wako tayari kuanza mapambano bila hofu.

“Tumekamilika na tumeridhika na timu yetu iliyosheheni vijana. Tupo tayari kwa mapambano na hili litathibitishwa Agosti nane tutakapocheza na Yanga, mtaona wenyewe namna timu ya kisasa inavyocheza,” alisema Ahmed.

Simba ilianza tena mazoezi Jumatatu na itaendelea na programu yake katika uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju, Dar es Salaam.

Leave a Comment