Soka

Dabi ya Kasi: Simba na Yanga Kuanza Msimu kwa Moto

Dabi ya Kasi: Simba na Yanga Kuanza Msimu kwa Moto

Alhamisi hii tunatarajia kushuhudia Dabi yenye kasi zaidi kutokana na jinsi vikosi vya Simba na Yanga vinavyocheza kwa kasi. Katika mchezo wa kirafiki dhidi ya APR, kocha Fadlu ameonyesha upendo wake kwa soka la kushambulia kwa kasi, ambapo wachezaji wake walivuka nusu ya pili ya uwanja kwa haraka na kushambulia kwa ufanisi.

Simba na Yanga: Ngao ya Jamii ni Dabi ya Kasi

Uwepo wa wachezaji wenye kasi kama Joshua Mutale, Mzamiru Yassin, Jean Charles Ahoua, Edwin Balua, Ladack Chasambi, Débora Fernandes Mavambo, na Awesu Awesu ulirahisisha kufika kwenye goli la wapinzani kwa haraka. Simba wameonyesha mabadiliko makubwa ya kiuchezaji, hata wanapokuwa hawana mpira wanajitahidi kuutafuta kwa haraka. Hii, pamoja na kasi ya Yanga kutoka nyuma hadi eneo la ushambuliaji, inatarajiwa kufanya mechi kuwa kali na ya kuvutia.

TATIZO SIMBA

Fadlu anakabiliwa na changamoto katika eneo la mwisho la ushambuliaji, ambalo limeonekana katika michezo minne ya kirafiki waliyoicheza. Kati ya mabao tisa waliyofunga, ni bao moja tu lililofungwa na mshambuliaji wa kati, Steven Mukwala. Wakiwa Misri kwa maandalizi ya msimu mpya, Fadlu alikiri kuwa na kazi ya kufanya katika eneo hilo.

Ingawa ni faida kuwa na wachezaji wa maeneo mengine wenye uwezo wa kufunga, kocha huyo anataka washambuliaji wake watumie nafasi wanazotengeneza kwa ufanisi. Akizungumzia Mukwala, kocha wa zamani wa Yanga na Azam FC, Hans van der Pluijm, anaamini mshambuliaji huyo anaweza kuwa suluhisho ndani ya kikosi cha Simba.

“Nimemwona akicheza Ghana, ni mshambuliaji mzuri sana. Wachezaji wengine huanza kuonyesha uwezo wao haraka, wengine huhitaji muda. Mukwala ana nguvu, kasi na maarifa,” alisema kocha huyo raia wa Uholanzi anayeishi Ghana.

SHIDA KWA YANGA

Yanga bado ina tatizo la kuzuia mipira ya juu, kama ilivyoonekana kwenye bao walilofungwa na Ricky Banda katika kilele cha Wiki ya Mwananchi. Banda alifunga kwa kichwa akiruka peke yake mbele ya Aziz Andabwile, aliyekuwa beki wa kati kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, akishirikiana na Dickson Job.

Kocha wa timu za vijana wa Azam FC, Mohammed Badru, alisema: “Tatizo hili lipo kwa timu nyingi za Tanzania, mwalimu (Gamondi) anatakiwa kulifanyia kazi.”

Leave a Comment