Soka

Sakata la Lameck Lawi: Simba na Coastal Union Wakutana

Lameck Lawi: Simba na Coastal Union Wakutana kwa Majadiliano

Viongozi wa Simba na Coastal Union walikusanyika Dar es Salaam kujadili sakata la usajili wa mchezaji Lameck Lawi ili kufikia makubaliano, kufuatia maagizo ya Kamati ya Hadhi na Sheria ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kamati hiyo ilitoa agizo la kikao hiki baada ya mkutano wake wa hivi karibuni kutokana na mvutano kuhusu usajili wa beki huyo. Simba ilitangaza kumsajili Lawi na kulipa fedha za usajili kwa Coastal Union, lakini viongozi wa klabu hiyo ya Tanga walikanusha taarifa hizo, wakidai Simba walikiuka makubaliano yao ya awali, hali iliyopelekea suala hilo kuwasilishwa kwa TFF.

Mwenyekiti wa Klabu ya Coastal Union, Steven Mguto, alieleza kuwa baada ya kikao hicho, majibu yatapelekwa kwa kamati hiyo ili waweze kutoa uamuzi wao.

“Simba na Coastal wanakutana mchana huu kuzungumzia suala la Lameck Lawi. Watakayokubaliana watayapeleka kwenye kamati ili itoe maamuzi yake,” alisema Mguto.

Mguto alifafanua kuwa kikao hicho kimeitishwa kwa maagizo ya kamati ya TFF, na hivyo wao (kamati) ndio watakaozungumza kulingana na makubaliano yatakayofikiwa na klabu hizo.

Kwa upande mwingine, Mguto alisema timu yao inaendelea na kambi ya mazoezi huko Visiwani Zanzibar, ikijiandaa kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC utakaochezwa Agosti 8 mwaka huu. Alieleza kuwa malengo yao ni kufanya vizuri katika mchezo huo wa ufunguzi wa msimu wa Ligi Kuu utakaonza Agosti 16.

“Malengo yetu ni kufanya vizuri katika michezo yetu yote, tukianzia na ule wa tarehe nane, kwani tuna imani kikosi tulichonacho kitafanya vema,” aliongeza Mwenyekiti huyo.

Leave a Comment