Yanga SC

Pacome Kuungana Na Yanga Kuikabili Kaizer Chiefs

Pacome Kuungana Na Yanga Kuikabili Kaizer Chiefs

Baada ya Pacome Zouzoua, kiungo mshambuliaji wa Yanga, kupewa siku tano kushughulikia pasipoti yake kabla ya kujiunga na wenzake kambini Afrika Kusini, taarifa zinaonyesha kwamba nyota huyo ameshawasili na huenda akashiriki mechi dhidi ya Kaizer Chiefs kesho.

Awali kulikuwa na taarifa kwamba Pacome angeweza kuja moja kwa moja jijini Dar es Salaam kutoka Ivory Coast alikoenda kushughulikia hati hiyo ya kusafiria wakati wenzake wakienda Afrika Kusini, lakini leo mchana viongozi wamekubaliana na kocha Miguel Gamondi kwamba aende moja kwa moja Sauzi.

Kocha Gamondi alisema kwamba alikusudia Pacome awasili Dar es Salaam kisha afanyiwe mazoezi ya ziada ili kwenda sambamba na wenzake, lakini kutokana na muda kuwa mdogo, ilibidi atue Sauzi jana mchana ili kujiandaa na mechi ya kesho ya Kombe la Toyota dhidi ya wenyeji, Amakhozi.

“Pacome yupo hapa Afrika Kusini, ameshaungana na wenzake kwa ajili ya mechi ya Jumapili dhidi ya Kaizer Chiefs, kisha tutarudi wote kuendelea na maandalizi ya mchezo mwingine wa kimataifa wa kirafiki katika Tamasha la Yanga na baadae mechi ya Ngao ya Jamii,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Tulipanga kukutana naye Dar es Salaam na nilimwandalia mazoezi maalum aliyotakiwa kuyafanya baada ya kukosa mechi mbili za awali za kirafiki zilizochezwa Mpumalanga. Angekuwa sawa tu na wenzake kwa utimamu wa mwili, lakini muda ulikuwa mdogo kwa kazi iliyopo mbele yetu, ndiyo maana ameungana na sisi huku.”

Gamondi alisema licha ya kukosa mazoezi na mechi hizo za awali huko Sauzi, bado anaamini kuwa Pacome ni mchezaji makini na hatakuwa na utofauti na wenzake. Aliongeza kuwa mashabiki wake wasiwe na wasiwasi kwani kutokuwepo kwake awali hakutapunguza chochote katika mchezo wake.

Pacome alikosa mechi dhidi ya Augsburg ya Ujerumani ambapo Yanga walipoteza kwa mabao 2-1, kisha kushinda bao 1-0 dhidi ya wenyeji wa michuano ya kimataifa ya Kombe la Mpumalanga, TS Galaxy.

Kesho Yanga itashuka tena uwanjani kuvaana na Kaizer Chiefs ya mjini Johannesburg katika mechi ya Kombe la Toyota, huku ikiwakutanisha na aliyewahi kuwa kocha wa kikosi hicho cha Jangwani, Nasreddine Nabi, aliyetua Kaizer akitokea FAR Rabat ya Morocco.

Baada ya mechi hiyo, Yanga itarudi kujiandaa na Tamasha la Kilele cha Wiki ya Mwananchi litakalofanyika Agosti 4 kabla ya kucheza na Simba katika Ngao ya Jamii kuzindua msimu mpya wa 2024-2025 siku ya Agosti 8 na atakayeibuka mbabe atacheza na mshindi wa mechi kati ya Azam FC na Coastal Union, Agosti 11.

Leave a Comment