Soka

Mokwena Ampa Sifa Fei Toto wa Azam FC

Mokwena Ampa Sifa Fei Toto wa Azam FC

Kocha Mkuu wa Wydad Casablanca ya Morocco, Rhulani Mokwena, ameonyesha kuvutiwa sana na uchezaji wa kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’. Mokwena ameeleza kuwa amegundua sifa za kipekee kwa Fei Toto, sio tu kwenye uwanja bali pia nje ya uwanja, akimwelezea kama mtu mwenye utu na upole tofauti na wachezaji wengi wenye vipaji kama vyake.

Baada ya mechi ya kimataifa ya kirafiki kati ya Wydad Casablanca na Azam FC iliyochezwa juzi huko Benslimane, Morocco, Mokwena alisema amekuwa akimfuatilia Fei Toto kwa muda na amevutiwa sana na uwezo wake. Hii ilikuwa mara yake ya kwanza kumuona mubashara uwanjani na aliguswa sana na uchezaji wake.

“Feisal ni mchezaji wa kipekee barani Afrika. Si tu kama mwanasoka, bali pia kama binadamu. Ana utu na upole ambao ni nadra sana kwa wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa kama vyake,” alisema Mokwena, ambaye msimu uliopita alikuwa kocha wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Katika mechi hiyo, Azam FC ilipoteza kwa mabao 4-1, ingawa hadi kipindi cha kwanza timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1. Mokwena alisifu Azam kwa kuonyesha mchezo mzuri na mgumu, ambao ulimsaidia kugundua mazuri na mapungufu ya kikosi chake.

“Naishukuru Klabu ya Azam kwa kunipa mechi nzuri. Ilikuwa mechi kali na yenye kasi kubwa. Nimeona uwezo wao na jinsi wanavyopambana, na kwa hili walilolionesha wanaweza kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Mokwena.

Azam FC tayari imeshacheza mechi tatu za kirafiki nchini Morocco. Awali walicheza dhidi ya US Yacoub Al Mansour na kushinda mabao 3-0, kisha wakacheza na timu ya Ligi Kuu, Union Touarga Sport na kutoka sare ya bao 1-1.

Leave a Comment