Simba SC

Kocha Fadlu Davids: Wiki Sita za Moto kwa Simba Kambini

Kocha Fadlu Davids: Wiki Sita za Moto kwa Simba Kambini

Kocha wa Simba Afichua Wiki Sita za Maandalizi Kabambe

Kocha wa Simba, Fadlu Davids, ameeleza kuwa baada ya wiki sita za maandalizi makali, timu yake itakuwa na uwezo mkubwa kwa msimu mpya. Alisema tayari wamekamilisha wiki tatu za mazoezi na wanajipanga kwa wiki tatu zilizobaki kukamilisha maandalizi yao.

Kocha huyo aliongeza kuwa usajili wa wachezaji wapya umekuwa mzuri, wakiwajumuisha wachezaji wenye vipaji na uelewa wa haraka. Alipongeza bodi ya klabu na rais kwa kufanya usajili wa wachezaji wachanga na wenye nguvu, ambao wamejumuika vizuri na wachezaji waliokuwepo.

“Nipongeze mfumo wa usajili, bodi ya klabu na rais. Tumepata kikosi kizuri chenye umri mdogo na nishati, wachezaji 14 wapya wakiungana na wengine 14 waliokuwepo. Ni wachezaji wenye vipaji na wana kitu cha kuonyesha,” alisema Davids.

Kocha Fadlu alisema wamebakiza wiki tatu za kumalizia kazi ya kuunda kikosi thabiti kwa msimu ujao. “Mimi ni kocha ambaye siwezi kutenganisha ufiti na mbinu. Tangu siku ya kwanza tulianza kufanyia kazi maandalizi ya kimbinu na kufanyia kazi jinsi tunavyocheza.”

Baada ya wiki sita, kocha huyo anaamini wachezaji watakuwa na staili ya kiuchezaji inayohitajika. Alisema kuwa baada ya mapumziko ya FIFA, watakuwa na mzunguko kamili na ushirikiano mzuri katika timu.

Akizungumzia mechi ya kilele cha tamasha la Simba Day dhidi ya APR kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Davids alisema mechi hiyo inalenga kuangalia maendeleo ya kiufundi na kufurahisha mashabiki.

“Tumeanza wiki ya nne ya maandalizi. Kuhusiana na utayari na maandalizi, tunaendelea. Mechi hii ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya na fursa kwa mashabiki kufurahia utambulisho wa wachezaji na benchi la ufundi,” alisema kocha huyo.

Leave a Comment