Simba SC

Kocha Fadlu Davids Awatumia Salamu Yanga

Kocha Fadlu Davids Awatumia Salamu Yanga

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameeleza matumaini makubwa kwa timu yake kupata mafanikio makubwa msimu wa 2024/25.

Simba, ikiongozwa na Fadlu kwa mara ya kwanza siku ya Simba Day, ilionyesha uwezo wake kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya APR FC baada ya kurejea kutoka kambi ya mazoezi nchini Misri. Katika mchezo huo, Simba ilishinda kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Debora Fernandez na Edward Balua, na kuwafanya mashabiki kuwa na matumaini makubwa kwa msimu ujao.

Baada ya ushindi huo, Simba sasa inaelekeza nguvu kwenye mchezo wa Nusu Fainali ya Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga Agosti 8, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Kocha Fadlu anaamini kuwa watafanya vizuri katika mchezo huo.

Fadlu alisema kuwa timu yake imekuwa ikiboresha uchezaji wake kwa kiasi kikubwa, akitolea mfano michezo ya kirafiki waliyocheza Misri na ule dhidi ya APR, ambayo yote walishinda.

“Naendelea kusuka kikosi imara kuelekea msimu ujao. Matarajio yangu ni kuchukua makombe msimu ujao kwa kushirikiana na benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki wetu. Nimefurahishwa na sapoti kubwa ya mashabiki niliyoiona kwenye Tamasha la Simba Day. Tupo tayari kwa mchezo wetu wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga,” alisema Fadlu.

Fadlu alisisitiza kuwa ataendelea kuboresha mapungufu yaliyogunduliwa katika michezo ya kirafiki katika siku chache zilizobaki kabla ya mchezo wa Ngao ya Hisani.

Leave a Comment