Soka

KMC Wadai Shilingi Milioni 200 kwa Awesu – Simba

KMC Wadai Shilingi Milioni 200 kwa Awesu - Simba

KMC Wadai Shilingi Milioni 200 kwa Awesu – Simba Wajikuta Matatani

Mwanasheria wa KMC FC na Mjumbe wa Bodi ya timu hiyo, Cheaf Said, amesema kuwa kiungo wao, Awesu Awesu, bado ni mchezaji halali wa KMC. Amefafanua kuwa Simba SC wanapaswa kurudi mezani kwa mazungumzo endapo wanamhitaji, wakiwa na ofa ya shilingi milioni 200.

Baada ya kikao chao na Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji, Cheaf alibainisha kwamba uamuzi wa kamati hiyo unatarajiwa hivi karibuni. Alieleza kuwa Awesu aliwasilisha barua ya kuomba kuvunja mkataba mnamo Julai 10, akidai kuwa anataka kwenda kukuza kipaji chake sehemu nyingine, lakini KMC walikataa ombi hilo mara moja.

Cheaf alifafanua kuwa sababu alizotoa Awesu hazikubaliki kwa mujibu wa mkataba, kwani hakukuwa na mazingira yoyote yaliyohalalisha kuvunjwa kwa mkataba, kama vile timu kushuka daraja au kushindwa kumpatia huduma muhimu. Hivyo, inaonekana wazi kwamba Awesu ameshawishiwa na Simba, ambao wanadai kumchukua kama mchezaji huru.

Cheaf alisema Simba walijaribu kuomba kibali cha kumtumia Awesu kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, lakini ombi hilo lilikataliwa kwa kuwa Awesu bado ana leseni inayosoma jina la KMC. Alisisitiza kwamba msimamo wa KMC ni kuwa Awesu arudi kwenye klabu, au Simba wawe tayari kulipa shilingi milioni 200 ili wamruhusu kuondoka.

Aliongeza kuwa awali walikuwa wamekubaliana Simba walipe shilingi milioni 70, lakini Simba walishindwa kufikia makubaliano hayo baada ya kutoa shilingi milioni 60 tu. Kwa sababu ya usumbufu huo, sasa wanataka shilingi milioni 200.

Leave a Comment