Simba SC

Joshua Mutale ajipatia jina “Mwamba wa Zambia”

Joshua Mutale ajipatia jina "Mwamba wa Zambia"

Winga mpya wa Simba, Joshua Mutale, sasa anajulikana kama Mwamba wa Zambia. Hii imewatia shauku mastaa wa zamani wa timu hiyo kumpa mbinu za kufanikiwa na kuendana na jina lake jipya.

Katika video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ya Simba, Mutale anaonekana akijiita Mwamba wa Zambia. Hapo awali, Clatous Chama, ambaye sasa yupo Yanga, alikuwa anajiita Mwamba wa Lusaka alipokuwa Simba.

Mutale anakiri kwamba Chama na Moses Phiri ndio walimfanya Simba kuamini katika uwezo wa wachezaji kutoka Zambia kutokana na mchango wao mkubwa ndani ya timu. Hii imempa motisha ya kufanya kazi kwa bidii ili kuandika historia yake mwenyewe na kuwapa nafasi wachezaji wengine wa Zambia kucheza Tanzania.

Straika wa zamani wa Simba, Athuman Machupa, alitoa ushauri kwa Mutale kwamba ili ajijengee ufalme ndani ya klabu, lazima kiwango chake kiwe na mchango mkubwa, huku akisisitiza nidhamu na kujituma.

“Soka linachezwa hadharani ambapo kila mtu anaona. Kama Chama alitikisa na jina lake la Mwamba wa Lusaka, na Phiri kwa jina la jenerali, naamini kwa umri wake, Mutale, akizingatia nidhamu na kujituma ataishi ndoto ya jina lake kuwa kubwa,” alisema Machupa.

Frank Kasanga ‘Bwalya’, mchezaji mwingine wa zamani wa Simba, alisema: “Bado hatujaona wachezaji wapya wanavyocheza, lakini kwa mechi nilizomuona, ni mchezaji mzuri. Ajitambue, kwani nidhamu ni kila kitu katika soka. Akifanya hivyo, atafanya makubwa na mashabiki watamwita Mwamba wa Zambia.”

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Danny Mrwanda, aliongeza kuwa heshima ya Mutale itajengeka endapo atafanya majukumu yake ipasavyo, kwani soka halina njia za mkato. Alisema kwamba akifanya kazi nzuri, mashabiki wanaweza kumpa jina lingine zaidi ya Mwamba wa Zambia.

Mutale aliwataka mashabiki wa Simba waunge mkono wachezaji wao katika majukumu yao. “Wapenzi wa Simba, mtuunge mkono, kwani Simba ni nguvu moja,” alisema.

Leave a Comment