Simba SC

Kocha Fadlu Davids Awakosoa Mutale na Mukwala

Kocha Fadlu Davids Awakosoa Mutale na Mukwala

SIMBA SC imemaliza kambi yao ya maandalizi ya msimu mpya nchini Misri baada ya wiki tatu, na leo Jumatano imerejea Dar es Salaam kujiandaa kwa Simba Day Jumamosi na msimu mpya utakaoanza Agosti 8 kwa mchezo wa Ngao ya Jamii.

Katika kipindi cha wiki tatu Misri, Kocha Mkuu Fadlu Davids ameangalia kwa undani kikosi chake baada ya kucheza mechi tatu za kirafiki na kushinda zote. Hata hivyo, licha ya ushindi huo, kocha Davids hajafurahishwa na namna safu yake ya ushambuliaji ilivyokuwa inapoteza nafasi nyingi za kufunga.

Joshua Mutale na Steven Mukwala, ambao ni wachezaji wapya, wamekutana na changamoto hiyo. Simba ilianza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Canal SC, ikashinda 2-1 dhidi ya Telecom Egypt, na kumalizia na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Al-Adalah FC.

Mbali na Mutale na Mukwala, wachezaji wengine wa safu ya ushambuliaji kama Valentino Mashaka na Freddy Michael wanapambana kurejesha heshima ya timu katika ligi baada ya kukosa taji la Ligi Kuu kwa misimu mitatu mfululizo.

Akizungumza kuhusu hali ya kikosi, Fadlu alisema anahitaji kufanya kazi kubwa kuhakikisha timu haipotezi nafasi nyingi za kufunga ili kushinda kwa mabao mengi. Alisema kuwa, licha ya changamoto hiyo, wachezaji wameanza kuingia kwenye mfumo wake wa mchezo.

“Timu imeimarika katika kila eneo na wachezaji wameanza kuendana na mfumo wangu. Shida ya kutofunga ni ndogo na inaweza kurekebishwa kwa muda mfupi kwani wachezaji wanajitahidi kujipanga vizuri kwenye nafasi,” alisema kocha Davids.

Kwa sasa, Simba inajiandaa kwa mechi ya Ngao ya Jamii na msimu mpya wa Ligi Kuu, ikitarajia kuonyesha mabadiliko makubwa na kurejesha taji la ligi baada ya kipindi cha ukame wa misimu mitatu.

Leave a Comment