HomeMichezoNabi na Gamondi Kupimana Nguvu Afrika Kusini

Nabi na Gamondi Kupimana Nguvu Afrika Kusini

NABI NA GAMONDI WAPIMANA NGUVU LEO AFRIKA KUSINI

Leo jioni, Klabu ya Yanga itakutana na Kaizer Chiefs kwenye Uwanja wa Bloemfontein nchini Afrika Kusini katika mechi ya Kombe la Toyota. Mashabiki wengi wa soka wanatarajia kushuhudia pambano kali la mbinu na ufundi kutoka kwa makocha Miguel Gamondi na Nasreddine Nabi.

Mashabiki wengi Tanzania na Afrika wanatamani kuona ni kocha yupi kati ya hao wawili, wenye mbinu za hali ya juu, ataibuka mshindi. Nabi, raia wa Tunisia, aliwahi kuifundisha Yanga na nafasi yake kuchukuliwa na Gamondi, raia wa Argentina. Makocha hao wameleta mafanikio makubwa kwa Yanga katika kipindi kifupi walichokaa na timu.

Nabi aliipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu kwa misimu miwili mfululizo na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Gamondi naye alipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita na kuifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nabi, ambaye alifundisha Yanga kuanzia 2021 hadi 2023 akitokea Al Merrikh ya Sudan, sasa ndiye Kocha Mkuu mpya wa Kaizer Chiefs. Alijiunga na timu hiyo akitokea FAR Rabat ya Morocco, alikokuwa baada ya kuondoka Yanga. Gamondi alichukua nafasi ya Nabi Yanga akitokea IR Tanger ya Morocco, na moja kwa moja akaifikisha Yanga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1998, na kuifikisha robo fainali, ikiweka rekodi ya kufika kwa mara ya kwanza tangu mfumo huo uanzishwe 1997.

Akizungumzia mchezo wa leo, Gamondi alisema haangalii sana matokeo bali anatilia mkazo kuona wachezaji wake wanafanya nini uwanjani kwa kufuata maelekezo yake na kujaribu mifumo mbalimbali watakayoitumia msimu huu.

“Tunafuraha kuwa hapa, tupo na wenzetu Kaizer Chiefs kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa za ‘Pre season’. Kwanza tunawashukuru mashabiki wetu kwa sapoti na kutushangilia katika mechi yetu ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mamelodi Sundowns. Tunacheza mechi ya kirafiki ambayo ni maandalizi ya msimu ujao. Tunaenda kuonyesha burudani, soka safi, tunachezesha wachezaji tofauti tofauti, siangalii sana matokeo bali timu inachezaje,” alisema Gamondi.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana mwaka jana, Julai 22, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, katika mechi ya tamasha la ‘Wiki ya Mwananchi’, Yanga ikishinda bao 1-0 lililofungwa na Kennedy Musonda. Mechi ya leo itakuwa ya tatu kwa Yanga tangu ifike Afrika Kusini, ambapo ilifungwa mabao 2-1 dhidi ya FC Augsburg ya Ujerumani Julai 21 kabla ya kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya TS Galaxy, Jumatano iliyopita.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Latest Posts