SIMBA YATAFUTA MRITHI WA LAKRED… MAZUNGUMZO NA MOUSSA CAMARA
Simba SC iko kwenye mazungumzo na klabu ya Horoya FC ya Guinea kwa ajili ya kumsajili golikipa wao, Moussa Camara, ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Guinea. Hatua hii inachukuliwa ili kuziba nafasi ya Ayoub Lakred aliyepata jeraha wakati wa mazoezi na anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki nne hadi sita.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa Simba inataka kumaliza dili hilo kabla ya kilele cha tamasha lao la kila mwaka la ‘Simba Day’ ifikapo Agosti 3, ili Camara mwenye umri wa miaka 25 awe miongoni mwa wachezaji watakaotambulishwa siku hiyo. Mtoa taarifa amesema kuwa ingekuwa inawezekana kumsubiri Ayoub apone, lakini kutokana na mechi nyingi muhimu za Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Tanzania na Ligi ya Mabingwa Afrika, hawataki kurudia makosa ya msimu uliopita ya kusubiri wachezaji wapone au wawe fiti.
“Ukweli ni kwamba Ayoub hayupo fiti kudaka kwa siku za hivi karibuni. Pamoja na madaktari kusema anaweza kupona baada ya wiki nne hadi sita, bado ameongezeka uzito. Kutokana na hilo, hata kama atarudi ndani ya muda huo, bado hatokuwa fiti kwa sababu atahitaji kuanza tena mazoezi ya kujiweka fiti, hivyo anaweza kukaa nje ya uwanja hata kwa miezi miwili. Hatuwezi kusubiri hilo kwa sababu tuna michuano mingi mikubwa na muhimu ambayo tunatakiwa tuanze vizuri,” alisema mtoa taarifa kutoka ndani ya Simba.
Imeelezwa kuwa iwapo dili hilo litafanikiwa, Simba inaweza kukata jina la Ayoub kwenye usajili wa Ligi Kuu na nafasi yake kuchukuliwa na Camara kwa sababu kanuni inaruhusu wachezaji wa kigeni 12 tu. Hata hivyo, jina la Ayoub linaweza kubaki kwa ajili ya mechi za kimataifa hadi kipindi cha dirisha dogo la usajili ambapo uamuzi mwingine unaweza kufanyika.
Kama Camara atafanikiwa kujiunga na Simba, atakuwa kipa wa pili kutoka Horoya ya Guinea kusajiliwa nchini Tanzania. Klabu ya Singida Black Stars tayari imemsajili golikipa Mohamed Kamara kutoka klabu hiyo hiyo. Tofauti yao ni kwamba golikipa wa Singida Black Stars anachezea timu ya taifa ya Sierra Leone, wakati Camara anachezea timu ya taifa ya Guinea.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa licha ya kutambulisha wachezaji wapya, bado hawajamaliza usajili, hivyo chochote kinaweza kutokea. Aliwataka wanachama na mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha la kilele cha Simba Day kwani kuna sapraizi za nguvu.
Leave a Comment