Ajira Tanzania

GGML Yatikiswa: RC Awaondoa Watumishi, Fedha za CSR Zazua Taharuki

GGML Yatikiswa: RC Awaondoa Watumishi, Fedha za CSR Zazua Taharuki

Geita. Mjadala mkali kuhusu fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Geita (GGML) umesababisha sintofahamu kubwa katika kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Geita. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, alilazimika kuwaondoa watumishi wa GGML baada ya majibu yao kutokuwa na mshiko kuhusu Sh9.2 bilioni zilizotakiwa kutolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo mwaka 2024.

Mvurugano huu ulianza baada ya Meneja Mwandamizi wa GGML, Gilbert Moria, kueleza kuwa mpango wa fedha hizo uliwasilishwa kwa Manispaa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita Februari 2024. Hata hivyo, kibali cha utekelezaji kilicheleweshwa hadi Novemba 2024, hali iliyoifanya kampuni kushindwa kuanza kutekeleza miradi kwa wakati.

Mwanasheria wa GGML, David Nzaligo, aliongeza kuwa ucheleweshaji wa halmashauri kuidhinisha mpango wa CSR ndio sababu ya fedha za 2024 kutotolewa, jambo lililomkasirisha RC Shigella. “Hakuna ujanja hapa, hizi ni fedha za wananchi, tokeni nje!” aliagiza kwa ukali, akisisitiza kuwa GGML inapaswa kurejesha fedha hizo kabla ya kuruhusiwa kushiriki tena vikao vya maendeleo.

GGML Yajibu Mashambulizi

Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti kwa Afrika, Simon Shayo, alifafanua kuwa Sheria ya Madini ya 2010 kifungu cha 105, pamoja na marekebisho ya 2017 na kanuni za 2023, zinaelekeza kuwa kampuni za uchimbaji zinapaswa kuandaa na kutekeleza mpango wa CSR kwa kushirikiana na jamii na mamlaka husika.

Shayo alieleza kuwa GGML iliwasilisha mpango wa CSR kwa mamlaka Februari 2024 lakini haukupitishwa hadi Novemba. Aidha, alisema kampuni hiyo haijapokea taarifa rasmi kutoka Manispaa ya Geita kuhusu hatua zinazofuata ili fedha hizo zitumike.

Mbunge wa Chato, Merdad Kalemani, alisisitiza kuwa sheria inazitaka kampuni kutekeleza miradi ya CSR kila mwaka bila kuchelewa, huku Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu, akihoji kwa nini GGML imefuta mpango wa 2024 badala ya kuutekeleza kama inavyotakiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, alitilia shaka gharama kubwa zinazotumiwa na GGML kwenye miradi ya CSR ikilinganishwa na miradi inayotekelezwa na Serikali. Alisema, “Chumba kimoja kinagharimu hadi Sh40 milioni, gharama hizi ni kubwa mno, tunahitaji mfumo mzuri wa utekelezaji wa miradi.”

Kwa sasa, sintofahamu hii inasubiri hatua zaidi, huku Serikali ikishinikiza GGML kuwajibika na kutoa fedha za CSR kwa maendeleo ya wananchi wa Geita.

Leave a Comment