Barcelona: Hali ya Sintofahamu Yaibuka, Flick Apata Presha
Wachezaji Waanza Kuonyesha Hasira Kwa Kukosa Muda wa Kucheza
Ingawa Barcelona ilipata ushindi wa kishujaa wa mabao 4-3 dhidi ya Celta Vigo siku ya Jumamosi, hali ndani ya klabu hiyo si shwari. Kocha Hansi Flick anazidi kujikuta kwenye presha kubwa huku baadhi ya wachezaji wake wakieleza wazi kutofurahishwa na maamuzi yake ya kiufundi.
Katika mchezo huo uliochezwa baada ya Barca kuwa nyuma kwa mabao 3-1 hadi dakika ya 60, timu hiyo ilirejea kwa kishindo na kushinda 4-3 kwa mabao mawili kutoka kwa Dani Olmo na Raphinha. Licha ya ushindi huo, hali ya sintofahamu inaendelea kutawala chumba cha kubadilishia nguo cha Blaugrana.
Ansu Fati Avuruga Mazingira kwa Hasira
Kwa mujibu wa Mundo Deportivo, Ansu Fati alikuwa mchezaji wa kwanza kuonyesha kutoridhika. Winga huyo kijana aliyekuwa akitarajiwa kuingia uwanjani, alionekana akifanya mazoezi pembeni lakini hakutumika. Aliporudi kwenye benchi, alikanyaga meza ya vinywaji, kutupa jezi yake na kupiga vifaa kwa hasira, akionyesha kutofurahia kutopewa nafasi ya kucheza.
Fati alikuwa anatarajia hiyo iwe mechi yake ya 10 msimu huu, lakini ndoto hizo zikayeyuka mbele ya macho yake.
Ferran Torres na Hector Fort Wafuata Nyayo
SPORT iliripoti kuwa dakika ya 60, muda mfupi kabla ya bao la tatu la Celta, Ferran Torres aliondolewa uwanjani na hakuficha hasira zake. Alipiga chupa ya maji chini na hakumsalimia Flick alipokuwa akitoka nje.
Baada ya filimbi ya mwisho, hali ya sintofahamu iliendelea pale beki kijana Hector Fort alipokataa kumsalimia kocha wake. Fort, mwenye miaka 18, amecheza mechi 14 msimu huu na kwa dakika chache, na kuonekana kutoridhika na nafasi anayopewa ndani ya kikosi.
Flick Akabiliwa na Mtihani Mgumu wa Udhibiti wa Kikosi
Hali hii inazua maswali kuhusu usimamizi wa Flick na uwezo wake wa kudhibiti kikosi chenye vipaji vingi lakini pia wachezaji wenye matarajio makubwa. Ikiwa hali hii haitadhibitiwa mapema, inaweza kuathiri mwenendo wa timu katika mbio za La Liga na michuano mingine.
Barcelona wanaonekana kuwa na nafasi nzuri ya kutwaa taji, lakini mgogoro wa ndani unaweza kuwa kikwazo kikubwa katika safari hiyo ya mafanikio.