Yanga Yamwongeza Djigui Diarra Mkataba Mpya wa Miaka Mitatu
Mchezaji mahiri wa Yanga, Djigui Diarra, amesaini mkataba mpya wa miaka mitatu, akibaki na timu hiyo hadi mwaka 2027. Tangazo hili lilifanyika wakati wa utambulisho wa wachezaji na benchi la ufundi la kikosi kwa ajili ya msimu ujao. Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, ndiye alitangaza habari hizi njema kwa mashabiki.
Diarra alijiunga na Yanga Agosti 2021, akitokea Klabu ya Stade Malien ya Mali. Tangu alipowasili, amekuwa mmoja wa makipa bora zaidi katika kikosi hicho, akichangia mafanikio mbalimbali ikiwemo kutwaa mataji ya Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii.
Kwa msimu uliopita, Diarra aliiongoza Yanga kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la FA. Kwa juhudi zake, alitunukiwa tuzo ya kipa bora wa FA katika tuzo za TFF zilizofanyika Agosti Mosi mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Diarra ataendelea kuwa nguzo muhimu kwa Yanga, akilenga kuisaidia timu kupata mafanikio zaidi katika misimu ijayo.