Michezo

Yanga Wajiandaa Kutamba Dhidi Ya Kaizer Chiefs… Gamondi Azungumza

Yanga Wajiandaa Kutamba Dhidi Ya Kaizer Chiefs… Gamondi Azungumza

Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2023/24, Yanga, wameweka nia thabiti ya kuwafunga Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa Toyota Cup. Klabu ya Yanga inafanya mazoezi katika viwanja vya St Stithians, Johannesburg, Afrika Kusini, chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, ambaye amesaini mkataba mpya wa mwaka mmoja kuongoza timu hiyo kwenye mashindano.

Mchezo huo utachezwa Julai 28, 2024, kama sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa 2024/25 unaotarajiwa kuanza Agosti 16. Miongoni mwa wachezaji waliopo kikosini ni Clatous Chama, Pacome, Aziz Ki, Prince Dube, Aboutwalib Mshery, Kibwana Shomari, Yao, na Jean Baleke.

Katika mechi mbili za kirafiki zilizopita, Yanga ilipata magoli kupitia kwa Jean Baleke katika mchezo wa kwanza na Prince Dube katika mchezo wa pili. Kocha wa klabu hiyo, Miguel Gamondi, amesisitiza kuwa lengo kuu la mechi za kirafiki ni kuona jinsi wachezaji wanavyotumia maelekezo wanayopewa badala ya kufikiria ushindi.

“Kwenye mechi zetu za kirafiki, tunazingatia zaidi jinsi wachezaji wanavyocheza na kufuata maelekezo tunayowapa mazoezini, kuliko kufikiria kushinda,” alisema Gamondi.

Yanga itakabiliana na Kaizer Chiefs katika mechi hiyo ya kirafiki Jumapili, kabla ya kurudi nyumbani kujiandaa na Kilele cha Wiki ya Wananchi Agosti 4.

Leave a Comment