Yanga Yapanga Mktaba Mpya Kwa Maxi Nzengeli
Kufuatia mafanikio makubwa ya Maxi Nzengeli nchini Afrika Kusini, mabosi wa Yanga wamemuita kwa mazungumzo ya mkataba mpya. Nzengeli anakaribia kumaliza mwaka wake wa mwisho wa mkataba wa miaka miwili aliosaini akitokea Union Maniema ya DR Congo.
Katika mechi tatu za kirafiki, Nzengeli ameonyesha kiwango cha juu, akiwavutia makocha wawili wakiwemo kocha wake, Miguel Gamondi. Mabosi wa Yanga wameanza kuchukua hatua za kumpa mkataba mpya wa miaka miwili kutokana na mchango wake mkubwa uwanjani.
Kiungo huyo ana nafasi kubwa kwenye safu ya kiungo ya Yanga kwa ubora wake wa kuzunguka uwanja mzima, akiwa eneo la ulinzi, kiungo, na hata kushambulia. Pia, Nzengeli anasifika kwa nidhamu kubwa ndani na nje ya uwanja.
“Tumeanza maandalizi ya kumpa mkataba mpya, tunamfuatilia kila kitu kuhusu wachezaji wetu,” alisema bosi wa juu wa Yanga. “Nzengeli ni mmoja wa wachezaji wenye nidhamu kubwa kwenye kikosi chetu, na ni heshima kwetu kubaki naye.”
Msimu uliopita, Nzengeli alimaliza na mabao 11, na mabosi wake walimzawadia mshahara mzuri na gari kutokana na kuanza vyema ndani ya timu hiyo.
GAMONDI ANASEMA NINI?
Kocha Gamondi alimsifu Nzengeli kwa kuwa mchezaji anayekimbia umbali mrefu na kuleta faida kubwa kwa timu. “Kuwa na Maxi kwenye timu yetu ni faida kubwa, ni mchezaji mwenye jitihada kubwa kuanzia mazoezini mpaka kwenye mchezo,” alisema Gamondi.
NABI NA MAXI
Kocha wa Kaizer Chiefs, Nasredine Nabi, alikiri kuwa Nzengeli ni mmoja wa wachezaji wa Yanga waliokipa shida kikosi chake kwenye upokonyaji wa mpira. “Kwenye mchezo ule alikuwa karibu kila eneo anapambana na kusukuma presha kwa wapinzani,” alisema Nabi.
KOCHA WA UNION MANIEMA
Papy Kimoto, kocha wa Union Maniema ya DR Congo, alisema Nzengeli anahitaji kuongeza utulivu kwenye eneo la kumalizia. Kimoto alieleza kuwa licha ya mabao 10, Nzengeli anahitaji kurudisha uwezo wake wa kupiga mashuti makali na ya mbali.
Nzengeli amefanikiwa kupenya kwenye hesabu kali za kocha Gamondi tangu alipotua Yanga, kutokana na uwezo wake wa kucheza kama winga, kiungo mshambuliaji na hata eneo la ulinzi.
Leave a Comment