Kukosekana kwa jina la kiungo wa Yanga, Khalid Aucho kwenye orodha ya wachezaji bora wa msimu wa 2023/24 kumezua mijadala mikali miongoni mwa wadau wa soka la Tanzania. Wengi wanaamini kuwa mchezaji huyo wa Uganda alistahili kuwemo katika orodha hiyo.
Sherehe za tuzo za Ligi Kuu Bara msimu uliopita zilifanyika Jumatatu, Agosti Mosi, jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Super Dome Masaki.
Kutojumuishwa kwa Aucho katika orodha ya wachezaji bora kumeibua mjadala, huku wengi wakilinganisha tuzo hizo na zile za mataifa yaliyoendelea, ikiwemo tuzo za mfungaji bora na kipa bora ambazo hazikuzua utata mkubwa.
Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua, alieleza kuwa Aucho alistahili kuwemo katika kikosi bora cha msimu kutokana na mchango wake mkubwa katika eneo la kiungo, akisema kuwa tofauti na Mudathir Yahya ambaye alitumika zaidi kushambulia, Aucho alikuwa muhimu kwa Yanga kama kiungo mkabaji.
“Mudathir ni mchezaji mzuri, lakini msimu uliopita hakutumika kama kiungo mkabaji. Aucho ndiye aliyestahili nafasi hiyo katika kikosi bora cha msimu,” alisema Chambua.
Nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella, aliheshimu maamuzi ya kamati ya tuzo, akisema kwamba vigezo vyao vya uteuzi vinapaswa kuheshimiwa na sio kukosolewa bila kuelewa undani wake.
“Nipo katikati, naweza kusema Aucho alistahili au hakustahili. Maamuzi ya kikosi bora yanajulikana na wanakamati,” alisema Mogella.
Kocha wa timu za vijana wa Azam FC, Mohammed Badru, aliongeza kuwa mbali na Aucho, Feisal Salum alistahili tuzo ya kiungo bora na kukubali uteuzi wa Stephane Aziz Ki kama mchezaji bora wa msimu.
“Kila mtu ana maoni yake, lakini tunapaswa kupongeza kamati kwa kazi nzuri waliyofanya. Mapungufu ni machache na naamini tuzo za msimu ujao zitakuwa bora zaidi,” alisema Badru.
Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, aliwataka wachezaji wa Tanzania kujituma zaidi, akisema kuwa wageni wengi wanatwaa tuzo kutokana na kujituma kwao.
“Ubora na uwezo wa Ibrahim Ajibu ni mkubwa, lakini Chama amekuwa akifanya vizuri zaidi kwa sababu anajua nini anafanya,” alisema Julio.
WASHINDI WA TUZO 2023/24
- Mfungaji Bora Kombe La Shirikisho la CRDB: Clement Mzize – Yanga
- Kipa Bora Kombe La Shirikisho la CRDB: Djigui Diarra – Yanga
- Mchezaji Bora Kombe La Shirikisho la CRDB: Feisal Salum – Azam FC
- Mfungaji Bora Ligi Kuu Bara 2023/2024: Stephan Aziz Ki – Yanga
- Kocha Bora Ligi Kuu Bara 2023/24: Miguel Gamondi – Yanga
- Mchezaji Bora Ligi Kuu Bara 2023/24: Aziz Ki – Yanga
- Beki Bora Ligi Kuu Bara 2023/24: Ibrahim Bacca – Yanga
- Kipa Bora wa Mwaka: Ley Matampi – Coastal Union
- Kiungo Bora wa Mwaka: Aziz Ki – Yanga
- Mchezaji Bora Chipukizi Ligi Kuu Bara: Shomary Raheem – KMC
- Mwamuzi Msaidizi Bora Ligi Kuu 2023/24: Mohammed Mkono
- Mwamuzi Bora Ligi Kuu 2023/24: Ahmed Arajiga
- Timu yenye Nidhamu: Mtibwa Sugar
- Kamishna Bora: Hamis Kitila – Singida
- Mchezaji Bora wa Tanzania anayecheza Nje (Me): Mbwana Samatta
- Mchezaji Bora wa Tanzania anayecheza Nje (Ke): Aisha Masaka
Leave a Comment