Junguni United Yaibua Sakata la Uchezaji Kamari
Uongozi wa klabu ya Junguni United inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) umewafukuza wachezaji saba kwa madai ya kujihusisha na michezo ya kubashiri matokeo (betting), kitendo kinachokiuka kanuni za ligi na maadili ya mchezo.
Walihusika Katika Mechi Mbili
Tuhuma hizo zinadaiwa kufanyika katika michezo miwili dhidi ya Malindi FC na New City, ambapo wachezaji hao waliripotiwa kubashiri matokeo ya mechi walizocheza.
Majina ya Wachezaji Waliosimamishwa
Wafuatao ndio wachezaji waliotimuliwa kutokana na tuhuma hizo:
- Salum Athumani ‘Chubi’
- Ramadhan Ally Omar ‘Matuidi’
- Abdallah Sebastian
- Danford Mosses Kaswa
- Bakari Athumani ‘Jomba Jomba’
- Rashid Abdalla Njete
- Idd Said Karongo
Uvunjifu wa Kanuni za Ligi
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa klabu hiyo, Suleiman Mwidani, wachezaji hao wamekiuka Katiba ya Junguni United pamoja na Kanuni za Ligi Kuu ya Zanzibar msimu wa 2024/2025, hasa kifungu namba 2 na 3, sura ya 23.
“Kulingana na sheria, mchezaji hatakiwi kubeti. Hivyo, wamekiuka sheria na wanapaswa kuchukuliwa hatua kali,” alisema Mwidani kupitia taarifa hiyo rasmi.
Wachezaji Wafungiwa Kujihusisha na Soka
Baada ya uchunguzi wa kina kufanywa na viongozi wa klabu, iliamuliwa kuwa wachezaji hao wasijihusishe na shughuli yoyote ya timu hiyo wala kushiriki katika mpira wa miguu, hadi hatua zaidi zitakapochukuliwa.
ZFF Yatajwa Kuombwa Kutoa Adhabu
Uongozi wa Junguni pia umetaka Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) kutoa adhabu kali kwa wachezaji hao ili liwe fundisho kwa wengine na kusaidia kupambana na tatizo la kamari katika soka la Zanzibar. (Chanzo: Mwanaspotii)