Elimu ya ngazi ya diploma imekuwa muhimu kwa maendeleo ya kitaifa nchini Tanzania. Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imejitolea kuhakikisha wanafunzi wenye sifa hawakosi fursa ya kuendeleza elimu kutokana na ukosefu wa fedha. HESLB inatoa mikopo ili kuwawezesha vijana wengi kupata elimu bora na kuchangia katika ujenzi wa taifa.
Mwongozo huu umetayarishwa kwa wanafunzi wa ngazi ya diploma kwa mwaka wa masomo 2024/2025, ukieleza vigezo, masharti, na mchakato wa maombi ya mkopo. Lengo ni kuhakikisha wanafunzi wanapata taarifa sahihi na kuelewa mchakato mzima wa maombi.
Vigezo vya Kupata Mkopo Ngazi ya Diploma
Sheria na Kanuni za Bodi ya Mikopo zinaainisha sifa kwa wanafunzi wanaohitaji mkopo baada ya kudahiliwa katika vyuo vyenye ithibati. Mwombaji atatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:
Vigezo vya Msingi vya Mwombaji Mkopo wa Diploma
- Awe Mtanzania mwenye umri usiozidi miaka 35 wakati wa kuomba mkopo.
- Awe amedahiliwa katika taasisi inayotoa elimu ya ngazi ya kati nchini.
- Awe amekamilisha na kuwasilisha maombi ya mkopo kupitia mfumo wa maombi ya mkopo (OLAMS).
- Asiwe na ajira au mkataba wa kazi serikalini au sekta binafsi.
- Awe amehitimu elimu ya Kidato cha Nne (CSEE), Cheti (astashahada) au Kidato cha Sita (ACSEE) ndani ya miaka mitano; yaani kati ya mwaka 2020 hadi 2024.
- Kwa mwanafunzi anayeendelea na masomo ahakikishe matokeo yake yametumwa Bodi kupitia Afisa Mikopo/uongozi wa Chuo.
Hali ya Kijamii na Kiuchumi
- Uyatima; aliyefiwa na mzazi au wazazi.
- Familia au kaya ya kipato duni inayofadhiliwa na Mifuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) au taasisi nyingine za kitaifa zinazotoa ufadhili.
- Ulemavu wa mwombaji au wazazi wake.
Nyaraka za Kuambatisha Wakati wa Maombi ya Mkopo
- Cheti cha kuzaliwa kutoka mamlaka husika.
- Vyeti vya vifo vya wazazi kuthibitisha uyatima.
- Barua kutoka RITA au ZCSRA kuthibitisha taarifa za kuzaliwa kwa waombaji waliozaliwa nje ya nchi.
- Fomu ya kuthibitisha ulemavu wa mwombaji au mzazi wake iliyoidhinishwa na Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) au Mkoa (RMO).
- Namba ya kaya ya Mnufaika kutoka TASAF kuthibitisha ufadhili wa kiuchumi.
Jinsi ya Kutuma Maombi ya Mkopo Ngazi ya Diploma 2024/2025
Mchakato wa kuomba mkopo wa HESLB kwa ngazi ya diploma ni rahisi na unafanyika mtandaoni. Hatua za kufuata ni hizi:
- Maombi Mtandaoni: Maombi yote yanafanyika kupitia Mfumo wa Maombi na Usimamizi wa Mikopo (OLAMS). Waombaji wanatakiwa kutumia namba ile ile ya Mtihani wa Kidato cha Nne iliyotumika wakati wa udahili.
- Ujazaji wa Fomu: Baada ya kuingia kwenye mfumo, jaza fomu ya maombi kwa usahihi na ukamilifu, na ambatanisha nyaraka zote zinazohitajika.
- Upakuaji na Saini: Baada ya kukamilisha maombi mtandaoni, pakua fomu za maombi na mikataba ya mkopo, gonga mihuri sehemu husika, saini fomu, na ambatanisha nyaraka zinazohitajika.
- Uwasilishaji wa Fomu: Wasilisha kurasa zilizosainiwa (nambari 2 na 5) kwenye fomu ya maombi katika OLAMS.
- Malipo ya Ada ya Maombi: Lipia ada ya maombi ya shilingi elfu thelathini (TZS. 30,000.00) kwa namba ya kumbukumbu ya malipo utakayoipata katika mfumo, kupitia benki au mitandao ya simu.
Leave a Comment