Victor Osimhen azungumzia hatma yake huku akihusishwa na vilabu vya EPL; Galatasaray yatamani abaki licha ya msimu bora Uturuki.
Victor Osimhen Afunguka Kuhusu Hatma Yake Galatasaray
Mshambuliaji hatari wa Kimataifa kutoka Nigeria, Victor Osimhen, ametoa kauli ya kwanza kuhusu hatma yake baada ya msimu mmoja wa mafanikio akiwa kwa mkopo ndani ya kikosi cha Galatasaray cha Uturuki.
Osimhen, ambaye alitokea Napoli kwa mkataba wa mkopo msimu uliopita, ameonesha kiwango cha juu msimu huu akifunga jumla ya mabao 29 kwenye mashindano mbalimbali, ambapo 21 kati ya hayo ni kwenye Ligi Kuu ya Uturuki. Mchango wake mkubwa umeisaidia Galatasaray kutwaa taji lao la 25, hatua iliyofanya jina lake kutikisa soko la usajili barani Ulaya.
Kutokana na ubora wake, vilabu vikubwa vya soka barani Ulaya vimeonyesha nia ya kumsajili, wakiwemo vigogo wa England kama Manchester United, Chelsea na Arsenal. Akizungumzia hali hiyo, Osimhen alisema: “Tutafanya uamuzi hivi karibuni. Itaamuliwa kitakachokuwa bora kwangu. Galatasaray itabaki moyoni mwangu daima. Leo ilikuwa siku isiyosahaulika kutwaa taji letu la 25.”
Kauli hiyo imetafsiriwa na mashabiki wengi kuwa ni dalili ya kuagana na Galatasaray, lakini Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Ibrahim Hatipoglu, amefafanua kuwa bado hakuna maamuzi rasmi yaliyofanywa na mchezaji huyo. Hatipoglu alisema: “Maneno yake hayamaanishi kuwa anaondoka. Alisema hata kama ataondoka katika dakika za mwisho Galatasaray itabaki moyoni mwake daima. Lakini hakusema kuwa anaondoka. Sisi tunataka abaki.”
Mbali na vilabu vya England, Osimhen pia anahusishwa na miamba ya Hispania, FC Barcelona, na miamba wa Italia, Juventus. Hata hivyo, ripoti zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 tayari amekataa ofa kutoka Juventus kwa sababu anapendelea kucheza katika Ligi Kuu England.
Hatma ya Osimhen inatarajiwa kuwekwa wazi mwishoni mwa msimu, lakini kwa sasa mashabiki wa Galatasaray wanaendelea kuwa na matumaini kuwa mshambuliaji wao tegemeo atasalia klabuni humo kwa msimu mwingine.