Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amefichua kwamba hakuna usajili ulioleta changamoto kwa viongozi wa klabu kama ule wa kiungo mshambuliaji wao, Kibu Denis. Taarifa hizi zinakuja wakati ambapo mchezaji huyo alikataa kujiunga na kambi ya klabu huko Misri na badala yake alielekea nchini Norway akidai kupata dili.
“Katika historia ya usajili wa Simba, hakuna uliotuletea shida kama huu wa kumuongezea mkataba Kibu Denis. Alikuwa anasema atapanua mkataba, lakini alitokeya huku na huko. Watu walikuwa wanamfuatilia kwa karibu. Hatukupata usingizi kwa wiki mbili,” alisema Ahmed Ally.
Ahmed aliongeza, “Watu wanasema Kibu ana goli moja, kweli ana goli moja lakini anajituma sana. Kibu ni aina ya wachezaji ambao wanacheza kwa moyo kama vile ni timu za familia zao. Hakuna timu inayotamani kukutana na Kibu.”
KLABU YATOA TAARIFA
Wakati taarifa zikieleza kuwa Kibu Denis, kiungo mshambuliaji wa Simba, ametorokea Norway, uongozi wa klabu umesema kuwa utamchukulia hatua za kinidhamu kwa kuwa alikimbia bila taarifa.
Taarifa hizi zinafuatia taarifa kwamba Kibu ametimkia Norway kimya kimya bila kutoa taarifa kwa klabu yake. Simba imeshikilia nyaraka zinazoonyesha kwamba Kibu ametimka nchini na sasa inashirikiana na uongozi wa mchezaji huyo ili kufuatilia hali hiyo.
Tukio hili limeibuka baada ya Kibu kuzua sintofahamu kwa kutorejea kazini baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili na kwenda Marekani kwa mapumziko ya mwisho wa msimu. Aliporejea nchini kutoka Marekani, Kibu hakuripoti kwa timu yake licha ya uongozi wa Simba, kupitia Meneja wa Habari Ahmed Ally, kuthibitisha kuwa klabu yao imechukua hatua nyingi za kumsaka ili ajiunge na wenzake katika kambi yao iliyoko jijini Ismailia, Misri.
Simba kwa sasa iko Ismailia kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, huku mchezaji huyo hadi sasa akiwa bado hajaripoti na taarifa zinadai kwamba ametimkia Norway. Taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ya klabu hiyo tarehe 23 Julai, imeeleza sababu za mchezaji huyo kutoshiriki katika kambi ya timu hiyo hadi sasa.
“Klabu ya Simba inautaarifu umma kwamba mchezaji wetu Kibu Denis Prosper hajafika kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mwaka 2024-2025.”
“Tunapenda kuutarifu umma kwamba Simba tulimwongezea mkataba Kibu kwa miaka miwili zaidi utakaomalizika Juni 2026 na kumlipa stahiki zake zote za kimkataba,” ilisema taarifa hiyo, ikiongeza;
“Hata hivyo, mchezaji huyu amekuwa akitoa sababu mbalimbali zinazomfanya kushindwa kuripoti kambini. Kutokana na utovu huu wa nidhamu, klabu itachukua hatua stahiki za kinidhamu na umma utapewa taarifa.”
Leave a Comment