Michezo

Stephane Aziz Ki kujiunga na Wydad Casablanca kwa Dau la Bilioni 2.5

Stephane Aziz Ki

Stephen Aziz Ki Ahamia Wydad Casablanca kwa Dau la Kihistoria

Kiungo Nyota wa Yanga SC Ajiunga Rasmi na Mabingwa wa Morocco

Kiungo mahiri wa Yanga SC, Stephane Aziz Ki, amefunga ukurasa wa safari yake ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuthibitishwa kujiunga na klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco. Taarifa kutoka ndani ya klabu zimeeleza kuwa mechi ya nusu fainali ya kwanza ya Kombe la CRDB Federation Cup dhidi ya JKT Tanzania ndiyo ilikuwa ya mwisho kwa nyota huyo akiwa na Yanga SC.

Aziz Ki amesajiliwa kwa ada ya takribani Shilingi Bilioni 2.5, na atakuwa analipwa mshahara wa milioni 80 kwa mwezi mara baada ya kujiunga rasmi na Wydad Athletic Club.

Usajili huu umetekelezwa haraka ili kuhakikisha kwamba Aziz Ki anakuwa sehemu ya kikosi cha Wydad Casablanca kitakachoshiriki michuano ya FIFA Club World Cup inayotarajiwa kuanza rasmi tarehe 15 Juni 2025.

Wydad Casablanca, ambao wamepewa nafasi ya kuiwakilisha Afrika kwenye michuano hiyo mikubwa, wanatarajia kuanza mazoezi yao tarehe 19 Mei. Mchezo wao wa ufunguzi utakuwa dhidi ya mabingwa wa Ulaya, Manchester City, mnamo Juni 18, 2025.

Uhamisho huu unakuja ikiwa ni miezi michache tu baada ya Aziz Ki kutwaa tuzo kadhaa za TFF, ikiwemo Kiungo Bora na Mchezaji Bora wa Mwaka 2024, hali inayoonesha thamani yake ndani na nje ya uwanja.

Uhamisho wa Stephane Aziz Ki kwenda Wydad Casablanca ni uthibitisho wa jinsi vipaji vya Tanzania vinavyoendelea kuvuka mipaka ya Afrika. Mashabiki wa Yanga SC wataendelea kumkumbuka kama mmoja wa wachezaji waliotoa mchango mkubwa katika mafanikio ya timu yao.

Leave a Comment