Stellenbosch Wakiwa Kwenye Moto Mkali, Simba SC Wana Kibarua Kigumu CAFCC
Kikosi cha Stellenbosch kutoka Afrika Kusini kinaonesha kiwango cha juu msimu huu, jambo linalowapa Simba SC mtihani mgumu kuelekea mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC). Stellenbosch kwa sasa wanashika nafasi ya tatu kwenye ligi kuu ya Afrika Kusini, wakifuatia timu kubwa kama Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates, hali inayothibitisha ubora wao ndani ya uwanja.
Moja ya wachezaji wa kutazamiwa zaidi ni beki wa pembeni Fawaaz Basadien, ambaye ana mchango mkubwa kwa timu. Basadien si tu mlinzi imara, bali pia ni hatari anapopanda mbele kwa kasi, akiwa na uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi za mashambulizi huku akitimiza majukumu ya ulinzi kwa mafanikio makubwa.
Mwingine mwenye ushawishi mkubwa katika kikosi hicho ni Devin Titus, ambaye anacheza kama winga wa kushoto. Devin ni mchezaji mwenye kasi, mbunifu na mwenye uwezo wa kushinda mipambano ya mtu kwa mtu kwa ustadi mkubwa. Simba wanapaswa kuwa makini naye kwani anaweza kubadilisha mwelekeo wa mchezo muda wowote.
Katika mashindano ya CAF msimu huu, Stellenbosch walipoteza michezo mitatu kwenye hatua ya makundi, dhidi ya RS Berkane mara mbili (nyumbani na ugenini), pamoja na kupoteza dhidi ya Stade Malien. Hata hivyo, kipigo hicho hakijaathiri mwenendo wao wa jumla kwani wameonesha uimara mkubwa kwenye mechi zao nyingine, jambo linalowafanya kuwa tishio kwa Simba SC.
Kwa mwenendo wa sasa wa Stellenbosch, ni wazi kuwa Simba SC hawatakutana na mchezo rahisi. Ubora wa wapinzani wao na motisha waliyonayo ya kufika fainali ya CAFCC unawafanya kuwa moja ya timu za kuogopwa Afrika kwa sasa. Simba SC italazimika kuwa makini na kufanya maandalizi ya hali ya juu ili kuhimili ushindani huo mkali.
Katika hatua ya nusu fainali, kila dakika uwanjani itakuwa muhimu, na Simba SC watalazimika kutumia uzoefu na mbinu bora ili kupata matokeo mazuri dhidi ya Stellenbosch ambao kwa sasa wapo kwenye kiwango cha juu kabisa.