Simbu Aweka Historia Boston Marathon 2025, Ashika Nafasi ya Pili

0
Simbu Aweka Historia Boston Marathon 2025

Alphonce Simbu Aing’ara Boston Marathon, Aweka Historia Mpya kwa Tanzania

Mwanariadha wa kimataifa kutoka Tanzania, Alphonce Felix Simbu, ameweka historia mpya kwa taifa baada ya kumaliza nafasi ya pili katika mbio za Boston Marathon zilizofanyika Aprili 21, 2025, huko Massachusetts, Marekani. Simbu alikamilisha mbio hizo za kilomita 42 kwa muda wa saa 2:05:04, akiwashangaza wengi kwa kuwapiku wanariadha waliotajwa kuwa na nafasi kubwa ya kushinda mashindano hayo ya kimataifa.

Simbu, ambaye ni Sajenti katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amekuwa Mtanzania wa pili kushika nafasi hiyo ya pili kwenye Boston Marathon, akifuata nyayo za Gabriel Geay aliyefanikisha hilo mwaka 2023. Mkenya John Korir ndiye aliyeibuka mshindi wa kwanza katika mbio hizo kwa muda wa saa 2:04:05, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Cybrian Kotut wa Kenya aliyemaliza kwa saa 2:05:08. Mmarekani Conner Mentz alimaliza wa nne kwa muda sawa na Kotut.

Kwa upande wa wanawake, Sharon Lokedi kutoka Kenya aling’ara kwa kushika nafasi ya kwanza kwa muda wa 2:17:22, akifuatiwa na Hellen Obiri (2:17:41), pia kutoka Kenya. Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Yalemzerf Yehualaw kutoka Ethiopia aliyemaliza kwa muda wa 2:18:06.

Meneja wa timu ya riadha ya JWTZ, Kapteni Christopher Masanga, alimpongeza Simbu kwa mafanikio hayo, akisema kuwa ni matokeo ya juhudi binafsi na mazingira wezeshi kutoka ndani ya jeshi. “Tumefurahi sana kama Jeshi kwa Mwanariadha wetu kufanya vizuri na kuiwakilisha nchi. Haya ni matunda ya JWTZ chini ya Mkuu wetu wa Majeshi kutoa nafasi kwa vijana wenye vipaji kuitangaza nchi kimataifa kupitia michezo,” alisema Kapteni Masanga.

Ushindi huo umeambatana na zawadi ya fedha inayokadiriwa kufikia Shilingi milioni 201.4, ambayo Simbu ameipata kwa kufanikisha kumaliza katika nafasi ya pili kwenye mashindano hayo maarufu duniani.

Matokeo ya Boston Marathon 2025

Wanaume

NafasiMwanariadhaTaifaMuda
1John KorirKenya2:04:05
2Alphonce SimbuTanzania2:05:04
3Cybrian KotutKenya2:05:08
4Conner MentzMarekani2:05:08

Wanawake

NafasiMwanariadhaTaifaMuda
1Sharon LokediKenya2:17:22
2Hellen ObiriKenya2:17:41
3Yalemzerf YehualawEthiopia2:18:06

Kupitia mafanikio haya, Alphonce Simbu ameendelea kuonyesha uwezo mkubwa wa wanariadha wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa, na kutoa hamasa kwa kizazi kijacho cha wanariadha nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here