Michezo

Simba Yatoa Masharti Mapya kwa Kibu Denis, Yataka Dola Milioni 1

Simba Yatoa Masharti Mapya kwa Kibu Denis

Simba SC imeweka sharti kali kwa mchezaji wake Kibu Denis pamoja na klabu ya Kristiansund BK inayomwinda ili kujiunga nayo katika Ligi Kuu ya Norway. Simba imeitaka Kristiansund BK kulipa Dola milioni 1 (Shilingi bilioni 2.7) kumnunua mshambuliaji huyo moja kwa moja, vinginevyo hawatakuwa tayari kumuachia kwa kiasi chochote chini ya hicho.

Kiongozi mmoja wa Simba ameieleza Mwananchi kuwa wamefikia uamuzi huu ili kutoa fundisho kuhusu umuhimu wa kuheshimu mikataba kwa wachezaji na klabu kama inavyotakiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

“Tumegundua makosa matatu makubwa katika suala hili la Kibu Denis. Kwanza, mchezaji aliiambia uongo klabu na kutoroka akijua ana mkataba wa muda mrefu. Pili, timu ya Norway ilifanya mazungumzo na mchezaji wetu kinyemela, jambo linalokwenda kinyume na kanuni za FIFA. Tatu, mchezaji ameiharibu taswira ya klabu kwa kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu kutokuwepo kwake kambini,” amesema kiongozi huyo.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa Simba imetoa sharti la kuvunja mkataba kwa dau la Dola milioni 1 na kwamba ikishindikana, watalishtaki suala hilo kwa FIFA.

“Tumesikia upande wa mchezaji ukijaribu kutuomba tumuuze kwenda Norway kwa dau wanalotaka wao, jambo ambalo si sawa. Msimamo wa klabu ni kwamba Kibu Denis anunuliwe moja kwa moja kwa Dola milioni 1 na sio kupelekwa kwa majaribio ya mwezi mzima kama wanavyotaka,” alifafanua kiongozi huyo.

Meneja wa Kibu Denis, Carlos Sylivester, alisema watakutana na Simba kutafuta suluhisho la tatizo hilo. “Kibu anapaswa kuelewa kuwa hawezi kuikwepa Simba kwani ana mkataba nao. Ni vizuri kukaa mezani na viongozi wake ili kutafuta suluhisho,” alisema Sylivester.

Sakata hili lilianza mwanzoni mwa mwezi uliopita baada ya Kibu Denis kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu na Simba, kisha kuomba ruhusa kwenda Marekani kwa ajili ya mapumziko. Hata hivyo, baada ya muda wa ruhusa kumalizika, Kibu hakujiunga na wenzake kambini Misri akidai hati yake ya kusafiria imeisha muda wake.

Simba walimwagiza kuwasilisha hati yake ya kusafiria ili iweze kuwekwa visa ya kuingia Misri, lakini alidai ameisahau Dar na hakuna mtu wa kuweza kuingia nyumbani kwake. Baadaye, ilibainika kuwa Kibu alienda Norway kwa mwaliko wa Kristiansund kufanya majaribio ya mwezi mmoja.

Leave a Comment