Klabu ya Simba imesitisha juhudi za kumsajili winga wa AS Vita Club, Elie Mpanzu, kutokana na matatizo mengi ya udanganyifu yaliyogundulika. Mpanzu sasa anatarajiwa kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji.
Habari kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa viongozi wa klabu hiyo wameamua kusitisha mawasiliano baada ya kugundua uwepo wa watu wengi wanaojitambulisha kama mameneja wa Mpanzu, kila mmoja akidai kuwa na mamlaka kamili juu ya mchezaji huyo. Hii imesababisha kucheleweshwa kwa usajili wa Mpanzu na kujiunga na timu kambini nchini Misri.
“Viongozi wa Simba wamefanya juhudi kubwa kukamilisha dili hili mapema. Awali walitoa ofa ya dola 200,000 za Kimarekani, lakini klabu ya AS Vita ilikataa na kutaka dola 250,000.
“Viongozi wa Simba hawakukata tamaa, baada ya kuondoka kwa Kibu Denis walirudi tena na kiasi kilichohitajika mara ya pili. Hata hivyo, kulikuwa na mkanganyiko wa fedha, klabu ya AS Vita inataka pesa, na klabu ya awali ya Mpanzu pia inadai sehemu yake ya ada ya usajili.
“Zaidi ya hayo, kulikuwa na mameneja kadhaa waliotaka kushiriki katika dili hilo baada ya kuona fursa. Hivyo, viongozi wa Simba walilazimika kusitisha mawasiliano na wote. Ukweli ni kwamba usajili wa Mpanzu umejaa udanganyifu, na msimamizi halali wa Mpanzu hajulikani. Viongozi wa Simba wameamua kujiepusha na matatizo haya,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa Simba inaweza kuingia tena sokoni kutafuta winga wa kulia kuziba nafasi ya Kibu Denis, ambaye ametoroka kwenda Norway. Tatizo la Kibu linaonekana kutokuwa na suluhu ya haraka, na kuna uwezekano wa kuuza mchezaji huyo kwa bei inayotakiwa na Simba au kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mchezaji na klabu iliyomrubuni.
Habari zaidi zinaeleza kuwa Mpanzu alikuwa tayari amekubali kujiunga na Simba kwa mshahara wa Shilingi milioni 26 za Kitanzania na ada ya usajili ya Shilingi milioni 323 za Kitanzania.
Kutokana na hali hiyo, Mpanzu sasa anatarajiwa kuhamia KRC Genk ya Ubelgiji baada ya usajili na Simba kushindikana.
Wakati hayo yakijiri, golikipa mpya wa Simba, Moussa Panpin Camara, alitarajiwa kufika nchini jana mchana ili kusaini mkataba wa kujiunga na timu hiyo.
Picha zilizotolewa jana na vyombo vya habari na mitandaoni nchini Guinea zilionyesha Camara akiwa na mabegi yake uwanja wa ndege tayari kwa safari ya kuja Tanzania.
Kipa huyo wa Timu ya Taifa ya Guinea anatoka Klabu ya Horoya FC na anakwenda kuchukua nafasi ya Ayoub Lakred, ambaye taarifa zinaeleza kuwa aliumia akiwa kwenye maandalizi ya msimu mpya nchini Misri.
Leave a Comment