Sifa za Kuomba Mkopo Elimu ya Juu 2024/2025
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ni taasisi muhimu inayotoa mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa Tanzania wenye uhitaji. HESLB, iliyoanzishwa chini ya Sheria Na. 9 ya mwaka 2004, inalenga kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye sifa anapata fursa ya kusoma bila kikwazo cha kifedha.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alitangaza kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2024/2025. Tangazo hili limeleta matumaini kwa wanafunzi wengi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu nchini.
Dkt. Kiwia alisisitiza waombaji kufuata miongozo ya utoaji mikopo iliyotolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda. Miongozo hii inapatikana kwenye tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) na inahusu vigezo vya utoaji mikopo kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza, stashahada, na shahada za umahiri.
Makala hii inatoa mwongozo kuhusu sifa na taratibu za kuomba mkopo wa HESLB ili kila mwanafunzi aweze kuelewa na kufuata vigezo vilivyowekwa.
Sifa za Kupata Mkopo wa HESLB 2024/2025
Sifa za Jumla
- Uraia: Mwombaji lazima awe raia wa Tanzania.
- Umri: Mwombaji awe na umri usiozidi miaka 35 wakati wa kuomba mkopo.
- Udahili: Ni sharti awe amedahiliwa katika taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa nchini Tanzania.
- Maombi kupitia OLAMS: Maombi yote yanafanywa kupitia Mfumo wa Maombi na Usimamizi wa Mikopo (OLAMS).
- Ukosefu wa kipato: Mwombaji hapaswi kuwa na chanzo kingine cha mapato kama vile ajira.
- Kurejesha mkopo uliopita: Aliyewahi kupokea mkopo wa HESLB ni lazima awe amerejesha angalau asilimia 25 kabla ya kuomba tena.
- Ufaulu wa masomo: Waombaji wawe wamehitimu elimu ya kidato cha sita au stashahada ndani ya miaka mitano.
Sifa za Msingi kwa Wanafunzi Wanaondelea na Masomo
- Ufaulu: Ni lazima wawe wamefaulu mitihani ili kuendelea na mwaka unaofuata wa masomo.
- Barua ya kurejea (kama inafaa): Kwa waliowahi kuahirisha masomo, wanapaswa kuwa na barua ya kurejea masomoni kutoka chuo husika.
- Kurudia mwaka: Hawaruhusiwi kurudia mwaka wa masomo zaidi ya mara moja.
- Kuahirisha masomo: Hairuhusiwi kuahirisha masomo kwa zaidi ya miaka miwili mfululizo.
- Namba ya Utambulisho ya Taifa (NIN): Lazima wawasilishe namba hii kabla ya kupokea fedha za mkopo katika mwaka wa tatu wa masomo.
Jinsi ya Kutuma Maombi ya Mkopo
Maombi yote ya mkopo yatafanyika kupitia Mfumo wa Maombi na Usimamizi wa Mikopo (OLAMS). Waombaji wanakumbushwa kutumia namba ileile ya Mtihani wa Kidato cha Nne iliyotumika wakati wa kuomba udahili.
Baada ya kukamilisha mchakato wa maombi mtandaoni, waombaji watapaswa kuchapisha (print) nakala za fomu za maombi na Mkataba wa Mkopo, kugonga mihuri sehemu husika, kusaini fomu, na kuzipakia kwenye mfumo wa OLAMS.
Mwisho wa Kutuma Maombi ya Mikopo
Dirisha la maombi ya mkopo kwa mwaka 2024/2025 litafunguliwa tarehe 01 Juni 2024 hadi tarehe 31 Agosti 2024. Mwongozo huu unapatikana kwenye tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz).
Leave a Comment