Yanga Yatinga na Ushindi wa 4-0 Dhidi ya Kaizer Chiefs
Yanga imeandika historia kwa kushinda taji lao la kwanza la Toyota Cup 2024 baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini. Siri ya ushindi huu imejikita katika falsafa ya timu kuona kila kitu ni muhimu kushinda ndani ya uwanja.
Ikumbukwe kwamba kocha wa Kaizer Chiefs, Nasreddine Nabi, aliwahi kuifundisha Yanga kabla ya nafasi hiyo kuchukuliwa na Miguel Gamondi. Gamondi alikuwa kwenye benchi la ufundi Julai 28, 2024, wakati Yanga walipotwaa taji hilo kwa mara ya kwanza, kama sehemu ya maandalizi ya msimu wa 2024/25.
Katika mchezo huo, mabao ya Yanga yalifungwa na Prince Dube dakika ya 25, Aziz Ki aliyefunga mabao mawili dakika ya 45 na 63, na Clement Mzize dakika ya 57.
Clatous Chama, kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga akitokea Simba, alieleza furaha yake kwa timu kupata ushindi huo. “Kwetu sisi kila kitu tunachukulia kwa umuhimu mkubwa, hivyo ushindi wetu na kupata kombe hili ni muhimu. Tunaamini ni mwanzo mzuri na tutazidi kupambana kufanya vizuri kwenye mechi zetu zote, mashabiki wazidi kujitokeza uwanjani kushuhudia burudani zaidi.”
Yanga inatarajiwa kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya mwendelezo wa maandalizi ya msimu wa 2024/25. Agosti 4, 2024, inatarajiwa kuwa Wiki ya Mwananchi, siku ambayo timu itafanya utambulisho wa wachezaji wapya na wale ambao walikuwa kwenye kikosi msimu wa 2023/24.
Leave a Comment