Michezo

Raisi Samia Apongeza Simba Day 2024 na Kutakia Heri Msimu Mpya

Raisi Samia Apongeza Simba Day 2024

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewatakia heri Simba SC katika msimu wa 2024-2025 na kuwapa ujumbe wa upambanaji. Raisi Samia, ambaye mwaka jana alikuwa mgeni rasmi kwenye Simba Day, mwaka huu alishindwa kuhudhuria kutokana na ziara ya kikazi.

Katika salamu zake hizo, Raisi Samia amewataka Wanasimba kusahau yaliyopita na kuangalia yajayo. Salamu hizi alizitoa kwa njia ya simu kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, wakati akizungumza na Wanasimba waliofika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika kilele cha Simba Day.

“Nawashukuru sana, nimerudi ziara sasa hivi nimefungua TV nimeona uwanja umejaa na shughuli zinaendelea. Nakumbuka mwaka jana tulikuwa sote hapo lakini mwaka huu limenipita lakini nikaona lisinipite kabisakabisa mpaka niongee nanyi.

“Mimi nawapongeza sana sana mmefanikisha vizuri siku ya Simba, najua mnajipanga vyema kwa msimu ujao na najua mmesajili vizuri. Wanasema yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

“Kwa hiyo mimi niwatakie kila la kheri,” alisema Raisi Samia.

Simba imefanya usajili wa wachezaji wapya 14, wakiwemo nane wa kimataifa na wazawa sita, ikiwa ni katika kuimarisha kikosi chao ili kuanza tena kubeba makombe ya Ligi Kuu na FA baada ya kuyakosa kwa takribani misimu mitatu mfululizo.

Leave a Comment