Opah Clement Ajiunga Na Henan Fc Ya Ligi Kuu Ya China
Mchezaji wa kimataifa wa Tanzania, Opah Clement, amejiunga na timu ya Henan Wanxian Mountain WFC inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake China akitokea Beşiktaş ya Uturuki. Opah, mwenye umri wa miaka 23, aliwahi kucheza Simba Queens kabla ya kuelekea Uturuki.
Akiwa Beşiktaş, Opah alijizolea sifa nyingi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao na kutawala uwanja. Kabla ya hapo, aliichezea klabu ya Kayseri Women ya Uturuki ambapo alifunga mabao matano katika mechi tano msimu wa 2021/22. Katika msimu wa 2023/24 wa Turkcell Women’s Football League, Opah alifunga mabao 12 katika mechi 10, na kuonesha uwezo mkubwa.
Henan Wanxian Mountain WFC inakabiliwa na changamoto kubwa katika ligi, ikiwa katika nafasi ya 11 baada ya mechi 13 bila ushindi, ikiwa na sare saba na kupoteza mechi sita. Timu hii imefunga mabao nane na kuruhusu mabao 21 kufungwa. Opah anatarajiwa kuleta mabadiliko na kusaidia timu yake mpya kupanda juu kwenye msimamo wa ligi. Mashabiki wa Henan Wanxian Mountain WFC wana matumaini makubwa kutokana na rekodi ya ufungaji ya Opah.
Wanawake wa Tanzania Katika Soka la Kimataifa
Opah sasa anaungana na kundi dogo la wachezaji wa kike wa Kitanzania wanaocheza nje ya Afrika, kama Clara Luvanga wa Al Nassr Women FC ya Saudi Arabia na Aisha Masaka wa Brighton Women FC ya England. Katika habari nyingine za uhamisho, Simba Queens wametangaza kumsajili kiungo mshambuliaji kutoka Nigeria, Precious Christopher, aliyewahi kucheza Yanga Princess na Rivers Angels FC ya Nigeria.
Leave a Comment