Winga wa Simba SC, Willy Onana, anatarajiwa kujiunga na klabu ya Muaither SC ya Qatar msimu ujao, licha ya timu hiyo kushuka daraja na sasa itashiriki Ligi Daraja la Kwanza. Onana ameuzwa kwa kiasi cha Dola 100,000 (zaidi ya Sh 250 Milioni), huku akipokea Dola 150,000 (zaidi ya Sh 300 milioni) kama malipo ya kujiunga na timu hiyo.
Muaither SC ilimaliza katika nafasi ya mwisho kati ya timu 12 zilizoshiriki Ligi Kuu ya Qatar msimu uliopita, baada ya kukusanya pointi 14 katika mechi 22. Timu hiyo ilishinda mechi tatu, ikatoka sare tano, na kufungwa mechi 14.
Onana alijiunga na Simba SC msimu uliopita akitokea Rayon Sports ya Rwanda, ambako alitambulika kama Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Rwanda (MVP). Hata hivyo, baada ya msimu mmoja tu, Onana ameamua kuondoka Simba kufuatia mabadiliko ya kikosi ambapo klabu hiyo imesajili wachezaji wapya akiwemo kipa Moussa Camara ‘Spider.’
Kuondoka kwa Onana kumekuja muda mfupi baada ya klabu hiyo kuamua kumleta kipa wa kigeni kufuatia kuumia kwa Ayoub Lakred, hatua ambayo iliwafanya Simba kutafuta mbadala.
Onana sasa anaungana na nyota wengine wa Simba waliotimkia timu nyingine katika dirisha hili la usajili, wakiwemo Clatous Chama, Henock Inonga, Sadio Kanoute, Babacar Sarr, Kennedy Juma, Israel Mwenda, John Bocco, na Saido Ntibazonkiza.
Leave a Comment