Michezo

Onana Aondoka Simba SC Kumpisha Moussa Camara

Willy Onana

Ujio wa kipa mpya kutoka Guinea, Moussa Camara ‘Spider’, umemfanya winga wa Simba, Willy Onana, kuondoka Msimbazi baada ya taarifa kuthibitisha kuwa atampisha kipa huyo aliyeletwa kuziba nafasi ya Ayoub Lakred aliyepata jeraha kambini Misri.

Taarifa ambazo Mwanaspoti ilizidokeza awali zimedhihirisha kuwa kipa huyo mpya mwenye mkataba wa miaka miwili ataingia kikosini huku Mcameroon, Onana, akitolewa.

Usajili wa Camara ni wa dharura kutokana na jeraha la Ayoub Lakred, ambaye alikuwa tegemeo katika kikosi hicho. Ujio wa Camara utaongeza ushindani kwa makipa wenzake Hussein Abel na Ally Salim.

Katika mazoezi ya mwisho ya timu hiyo yaliyofanyika leo Ijumaa, Agosti 2, 2024, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Onana hakuwa sehemu ya kikosi. Taarifa za ndani zinaeleza kuwa tayari amepata timu huko Qatar anayoweza kujiunga nayo wakati wowote.

Mwanaspoti ilikuwa ya kwanza kuripoti kwamba endapo dili la Camara likikamilika, Onana ataondolewa na hicho ndicho kilichotokea.

“Onana hatakuwa sehemu ya timu kwa msimu ujao. Tumefanya hivyo ili kusalia na wachezaji 12 wa kigeni. Bahati nzuri alikuwa analijua hilo tangu tupo Misri kwenye maandalizi ya msimu mpya,” alisema kiongozi mmoja wa timu hiyo.

Simba ilimsajili Onana msimu uliopita kutoka Rayon Sports ya Rwanda akiwa mchezaji bora wa ligi kuu nchini humo (MVP).

Leave a Comment