Wachezaji wapya wa Simba SC, Joshua Mutale (winga) na Steve Mukwala (mshambuliaji), wameelezea uzoefu wao kwenye kambi ya timu huko Ismailia, Misri.
Joshua Mutale alieleza kuwa walifurahia muda wao Misri wakijiandaa kwa msimu mpya. Alisisitiza kuwa wameimarika kimwili na kiushindani, na sasa wako tayari kukabiliana na changamoto za msimu ujao. Mutale pia alifurahia ushirikiano mzuri kati ya wachezaji wenzake, akisema kuwa kuna muunganiko thabiti katika kikosi.
Kwa upande wake, Steve Mukwala, ambaye alifunga goli moja kwenye mechi ya mwisho ya kirafiki, alisema maandalizi yamekuwa mazuri sana. Ameona jitihada za wachezaji wenzake wakipambana kutafuta nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Mukwala aliwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi Jumamosi katika Simba Day, akiwahidi burudani ya hali ya juu.
Simba walicheza mechi tatu za kirafiki wakiwa Misri, wakifunga mabao saba na kuruhusu mawili tu. Wafungaji wa mabao hayo walikuwa ni Mutale, Mukwala, Mashaka, Ladack Chasambi, Augustine Okejepha, na Charles Ahoua aliyepiga mabao mawili.
Leave a Comment