Moussa Camara Ajiunga na Simba SC kwa Mkataba wa Miaka Miwili
Klabu ya Simba imemtambulisha rasmi mlinda lango wao mpya, Moussa Camara ‘Spider’, aliyesaini mkataba wa miaka miwili akitokea AC Horoya ya Guinea. Camara, ambaye ni maarufu kwa jina la Spiderman kutokana na umahiri wake wa kudaka mipira, ni raia wa Guinea mwenye umri wa miaka 25.
Camara amejiunga na Simba kuongeza nguvu katika eneo la ulinzi baada ya Ayoub Lakred kuumia akiwa kambini jijini Ismailia, Misri. Baada ya kusaini mkataba, kipa huyo ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Guinea, ameonyesha shukrani zake kwa uongozi wa Simba kwa kumpa nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo.
“Nashukuru sana kuwa hapa Simba, ni timu kubwa ambayo wachezaji wengi Afrika wanatamani kuichezea. Namshukuru Mungu na viongozi wa Simba kwa kunipa nafasi hii na kuniamini,” alisema Camara na kuongeza kuwa yupo tayari kushirikiana na wachezaji wenzake kuhakikisha timu inapata mafanikio.