Michezo

Manula na Onana Waachwa Simba

Manula na Onana Waachwa Simba

Katika hatua za kushangaza, aliyekuwa kipa namba moja wa Simba, Ashi Manula, ametemwa kutoka kwenye kikosi cha msimu ujao wa 2024/25. Hii ni baada ya timu hiyo kutambulisha makipa wanne wapya na jina la Manula likakosekana.

Akizungumza katika tamasha la Simba Day lililofanyika Uwanja wa Mkapa, Afisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, aliorodhesha majina ya makipa watakaokuwa sehemu ya kikosi hicho. Makipa hao ni Ally Salim, Ayoub Lakred, Mohammed Camara, na Hussein Abel. Majina haya yaliibua shangwe miongoni mwa mashabiki waliokuwepo uwanjani, hasa kwa kutajwa kwa Lakred ambaye inaripotiwa atakuwa nje kwa miezi sita kutokana na jeraha alilopata akiwa mazoezini.

Aishi Manula
Aishi Manula

Shangwe kubwa pia zilisikika baada ya kipa mpya kutambulishwa, ambaye amesajiliwa kuziba pengo la Lakred wakati akiwa anauguza jeraha lake. Ahmed Ally alithibitisha kwa kusema, “Hawa ndio walinda mlango ambao tutakuwa nao msimu ujao.”

Mchezaji mwingine ambaye ametemwa rasmi ni Willy Essomb Onana. Jezi yake namba 7 sasa imechukuliwa na Joshua Mutale. Inaelezwa kuwa Onana tayari amepata timu mpya nje ya Afrika na amefikia makubaliano na klabu hiyo.

Tukio hili limeacha maswali mengi kwa mashabiki wa Simba, huku wengi wakisubiri kuona jinsi kikosi kipya kitakavyofanya msimu ujao.

Leave a Comment