Mvutano wa kisiasa Sudan Kusini umechukua sura mpya baada ya vikosi vya usalama kumkamata Waziri wa Mafuta na maafisa waandamizi wa jeshi wanaoshirikiana na Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar. Tukio hili limeongeza hofu ya kuyumba kwa makubaliano ya amani yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Katika mji mkuu wa Juba, wanajeshi walimzingira Machar nyumbani kwake, huku Naibu Mkuu wa Jeshi, Jenerali Gabriel Duop Lam, akizuiwa Jumanne iliyopita. Siku iliyofuata, Waziri wa Mafuta, Puot Kang Chol, alikamatwa pamoja na walinzi wake na familia yake.
Machar, ambaye uhasama wake wa muda mrefu na Rais Salva Kiir umesababisha migogoro mikubwa ya kisiasa, aliwahi kutahadharisha kuwa kufukuzwa kwa washirika wake serikalini kunaweza kuhatarisha makubaliano ya amani ya mwaka 2018. Makubaliano hayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano, ambapo zaidi ya watu 400,000 walipoteza maisha.
Msemaji wa chama cha Machar, SPLM-IO, Pal Mai Deng, alieleza kuwa kukamatwa kwa Lam kunahatarisha amani na kuvuruga Bodi ya Ulinzi ya Pamoja, taasisi muhimu katika utekelezaji wa mkataba huo. “Hatua hii inavunja Mkataba wa Amani na inaathiri amri na udhibiti wa vikosi,” alisema Deng.
Mbali na kukamatwa kwa maafisa hao, wanajeshi wa Jeshi la Sudan Kusini (SSPDF) waliripotiwa kuwekwa karibu na makazi ya Machar, jambo lililoibua taharuki. Puok Both Baluang, msemaji mwingine wa Machar, alisema kuwa baadhi ya maofisa wa kijeshi wanaomuunga mkono Machar wamewekwa katika kizuizi cha nyumbani bila sababu yoyote kutolewa.
Hata hivyo, msemaji wa jeshi, Meja Jenerali Lul Ruai Koang, alikataa kutoa maoni kuhusu hali hiyo.
Mvutano huu unaonekana kuchochewa na hali tete katika jimbo la Upper Nile, ambapo SSPDF inamtuhumu Lam na vikosi vyake kwa kushirikiana na waasi wa White Army, kundi linalohusiana na kabila la Nuer.
Sudan Kusini ilijipatia uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011, lakini miaka miwili baadaye, taifa hilo liliingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya Kiir kumtimua Machar. Vita hivyo viliwalazimisha watu milioni 2.5 kukimbia makazi yao na kusababisha njaa kali kwa karibu nusu ya raia wa nchi hiyo.
Ter Manyang Gatwich, mkurugenzi wa Kituo cha Amani na Utetezi, ametoa wito wa kuachiliwa huru kwa waliokamatwa ili kuepusha hali mbaya zaidi ambayo inaweza kusababisha machafuko mapya na umwagaji damu.
Leave a Comment