Man United kumkosa Leny Yoro kwa miezi mitatu
Manchester United itamkosa beki wake mpya, Leny Yoro, kwa muda wa miezi mitatu baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kushoto. Yoro (18) alipata maumivu ya enka katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Arsenal, Julai 28, yaliyotarajiwa kumweka nje kwa wiki sita.
Hata hivyo, mambo yamebadilika na sasa beki huyo aliyesajiliwa kutoka Lille ya Ufaransa majira haya ya kiangazi, atakuwa nje kwa miezi mitatu. Jumatatu iliyopita, Yoro alifanyiwa upasuaji huo na klabu yake imethibitisha kuwa atakosekana kwa miezi mitatu akiuguza majeraha.
“Tuna matarajio atarejea ndani ya miezi mitatu,” ilifafanua taarifa ya Man United. Yoro mwenyewe amewashukuru mashabiki kwa jumbe za kumtakia heri.
“Huu sio mwanzo nilioutarajia lakini ndio hali ya mpira. Upasuaji umeenda vizuri, asanteni kwa sapoti yenu. Sasa ni wakati wa uvumilivu na kazi ya ukarabati. Tutaonana muda mchache ujao nikiwa imara,” alisema Yoro.
Yoro alinunuliwa kwa ada ya Pauni milioni 52 kutoka Lille, Julai 18 na hadi sasa amecheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Rangers na Arsenal.
Leave a Comment