Michezo

Lameck Lawi Afanya Mazoezi Ubelgiji, Simba Wapatana Na Coastal

Lameck Lawi Afanya Mazoezi Ubelgiji, Simba Wapatana Na Coastal

Baada ya Kamati ya Usuluhishi ya TFF kuelekeza Simba na Coastal Union kutatua mgogoro wao kwa mazungumzo ya busara, viongozi wa timu hizo walikutana Julai 27 kujadili hatima ya Lameck Lawi ambaye kwa sasa yupo Ubelgiji, akifanya vipimo na klabu ya K.A.A Gent inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji.

Mpango wa Lawi kujiunga na Simba ulikwama baada ya viongozi wa Coastal kuvunja makubaliano na Simba kwa madai ya kucheleweshwa malipo, na hivyo mchezaji huyo kusafiri hadi Ubelgiji kutafuta nafasi ya kusajiliwa. Ikiwa dili litakamilika, Lawi atakuwa Mtanzania wa tatu kucheza huko baada ya Mbwana Samatta na Kelvin John ‘Mbappe’ waliowahi kucheza KRC Genk.

Akiwa Ubelgiji, Lawi alizungumza kwa njia ya simu na kusema kuwa vipimo vilikwenda vizuri na ameanza mazoezi na timu hiyo. Aliongeza kuwa: “Naendelea vizuri na tayari nimeanza kufanya mazoezi na timu hii. Nafikiri suala la mimi kuuzwa au kufanya majaribio wenye nafasi nzuri ya kuzungumza ni viongozi.”

Lawi alieleza kuwa anafanya kazi aliyokuja nayo, ambapo baada ya vipimo kukamilika, sasa yupo kwenye hatua ya pili ya mazoezi.

Lawi, ambaye msimu uliopita alionyesha uwezo mkubwa katika nafasi ya beki wa kati na kusaidia timu yake kumaliza katika nafasi ya nne na kupata nafasi ya uwakilishi katika Kombe la Shirikisho Afrika, amekuwa Ubelgiji kwa wiki sasa.

Wakati Lawi akiwa Ubelgiji, Simba ambao wanatajwa kufikia makubaliano naye katika dirisha hili la usajili, wanasubiri hatma ya kumnasa mchezaji huyo kutoka Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, ambayo itakutana wiki moja kabla ya dirisha kufungwa. Coastal Union wanasema kuwa Lawi bado ni mchezaji wao.

Leave a Comment