Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameeleza kusikitishwa kwake na washambuliaji wa timu yake kushindwa kutumia nafasi nyingi wanazozitengeneza na kugeuza kuwa magoli. Ingawa timu yake ilishinda mechi mbili mfululizo za kirafiki, Fadlu ameonyesha wasiwasi kuhusu uwezo wa washambuliaji kumalizia nafasi hizo.
Simba ilianza kwa kucheza na Canal SC na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, kisha ikashinda mabao 2-1 dhidi ya Telecom Egypt siku ya Jumapili. Jana, walikuwa na kibarua cha kukabiliana na Al-Adalah FC kutoka Saudi Arabia.
Fadlu alisema, “Hadi sasa tumeboresha maeneo mawili, utimamu wa mwili na kuwajenga wachezaji kisaikolojia. Shida iliyopo ni jinsi ya kutumia nafasi, lakini hilo sio gumu kwani kama wanaweza kutengeneza nafasi, kutumia ni suala la muda.”
Aliendelea kusema, “Wametengeneza nafasi nyingi lakini wanashindwa kuzitumia. Hili halinipi wasiwasi sana kwani licha ya kukosa, bado wanakuwa kwenye maeneo sahihi kupambana.”
Fadlu aliongeza kuwa timu imeimarika kila eneo na wachezaji wameanza kuingia kwenye mfumo. Shida ya kutofunga ni sehemu ndogo ambayo inaweza kutatuliwa kwa muda mfupi kwani wachezaji wamekuwa wakijitenga vizuri kwenye nafasi.
Kocha huyo, ambaye alichukua nafasi ya Abdelhak Benchikha, amesema kuwa kwa muda waliokaa Misri tayari ameshuhudia mabadiliko makubwa kwenye kikosi na anaamini hadi watakaporudi Dar, atakuwa amejenga kikosi bora. “Simba Day itaeleweka na ligi ikianza kila kitu kitajulikana,” alisema Fadlu Davids.
Leave a Comment