Kocha Mkuu wa Red Arrows ya Zambia, Chisi Mbewe, amesema mwaliko wa kucheza na Yanga katika kilele cha ‘Wiki ya Mwananchi’ ni fursa nzuri kwao, kwani wanakutana na timu imara itakayowapa changamoto mpya. Timu hiyo, mabingwa wa Ligi Kuu ya Zambia (ZPL), inatarajiwa kuwasili hivi karibuni kwa ajili ya mchezo huo muhimu utakaofanyika Jumapili, Agosti 4, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mbewe alisema, “Tunaenda kukutana na timu nzuri ambayo itakuwa ni kipimo kizuri kwetu, hasa wakati huu wa maandalizi ya msimu ujao. Hatukuweza kukataa mwaliko huu kwa sababu tunaamini Yanga pia ni mabingwa na watatupa ushindani.”
Kocha huyo aliongeza kuwa anaiheshimu Yanga kwa sababu ni timu bora yenye wachezaji wazuri, na hivyo anakuja na kikosi kamili kwa mchezo huo, akisisitiza kuwa ni sehemu ya maandalizi muhimu kwa msimu ujao. “Yanga ni timu kubwa na bora, hivyo tunaweza kuuita mchezo wa mabingwa. Utatusaidia kuona mapungufu yetu na jinsi ya kuyarekebisha, kama ilivyokuwa pia kwenye michuano ya Kagame.”
Red Arrows inatarajiwa kutua nchini muda wowote kwa ajili ya mchezo huo, huku ikiwa tayari imeongeza winga Mkongomani, Emmanuel Bola Lobota, aliyekuwa akiwindwa na Yanga kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Singida Black Stars.
Mbali na ubingwa wa Zambia, Red Arrows pia ni mabingwa wa Kombe la ABSA 2024, na walichukua Kombe la Kagame mwaka huu jijini Dar es Salaam baada ya kuifunga APR ya Rwanda kwa penalti 10-9 kufuatia sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120.
Leave a Comment