Kocha Mkuu wa Singida Black Stars (SBS), Patrick Aussems, amesema bado anaendelea kusuka kikosi cha ushindani kwa kutumia mechi za kirafiki huku akidai timu hiyo ipo tayari, lakini kazi ni kwake kusaka kikosi cha kwanza.
Aussems alieleza hayo baada ya timu yake kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Dodoma Jiji, ambapo alisema ameanza kusuka safu ya ushambuliaji kabla ya kumalizana na mabeki.
“Tumepata fursa nzuri ya kushiriki Kagame Cup. Licha ya timu kutokuwa na maandalizi ya kutosha, mashindano hayo yametuonyesha ni maeneo gani tuna upungufu,” alisema kocha huyo na kuongeza:
“Katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji, sikuangalia sana matokeo, nilipanga kikosi kwa kujaribu mfumo tofauti ambao nitaweza kuutumia baada ya ligi kuanza. Nilianza na washambuliaji wawili kwa lengo la kuwajenga.”
Aussems alisema kuwa safu ya ushambuliaji ipo vizuri katika kutengeneza nafasi, lakini tatizo ni umaliziaji. Kwa mchezo ujao dhidi ya Namungo FC, Agosti Mosi, atatumia mshambuliaji mmoja na mfumo wa kujilinda ili kubaini upungufu wa ukuta wake.
“Nitafanya hivyo kwa lengo la kuona sehemu gani ukuta wangu una shida na nini natakiwa kuboresha kabla ya ligi kuanza ili kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuonyesha ushindani kwa wapinzani,” alisema.
Kocha huyo, ambaye aliwahi kuinoa Simba, na sasa amejiunga na Singida Black Stars, alisema kwa ujumla kikosi chake kipo kwenye nafasi nzuri ya ushindani na kilichobaki ni kupambana kusaka kikosi cha kwanza.
“Wachezaji wengi wameonyesha wanahitaji namba kikosi cha kwanza na wapo kwenye utimamu mzuri wa kimwili. Kazi ni kwangu mimi kuamua nani ataanza na nani atacheza kikosi cha pili,” alisema.
Singida Black Stars, mbali na mechi za Kombe la Kagame, hadi sasa imecheza mechi tatu za kirafiki ikianza na Polisi Tanzania ikashinda 3-0, dhidi ya ACA Eagles sare ya mabao 2-2 na kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Dodoma Jiji.
Leave a Comment